WATUMISHI WAPYA BRELA WATAKIWA KUFANYIA KAZI MAFUNZO WALIYOPEWA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 24, 2022

WATUMISHI WAPYA BRELA WATAKIWA KUFANYIA KAZI MAFUNZO WALIYOPEWA.



Na Mwandishi wetu Dar-es-salaam 

Afisa Mtendaji Mkuu wa wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) amewataka watumishi wapya kutekeleza kwa vitendo mambo yote waliyofundishwa ili kuleta ufanisi kwenye jamii wanayoihudumia.

Bw. Nyaisa ametoa wito huo mapema leo tarehe 23 Mei, 2022, wakati wa kufunga mafunzo ya siku tano kwa watumishi wapya wa BRELA, yaliyofanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Njia ya Mtandao, kilicho chini ya Chuo cha Utumishi wa Umma jijini Dar es Salaam.

Bw. Nyaisa amesema kuwa ili taasisi hiyo iweze kuendelea, watumishi hao 
wanapaswa kutumia ujuzi wao kwa kujituma kazini na kuwa wabunifu zaidi ili kufikisha huduma bora kwa wadau.

Ameongeza kuwa ajira na mafunzo yanayotolewa na Serikali lengo kuu ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini.   

Pia Bw. Nyaisa amesisitiza suala la uadilifu mahala pa kazi na kuepuka urasimu ambao unaweza kuleta taswira mbaya kwa taasisi.
" Kila mmoja ana jukumu la kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuleta matokeo chanya ya kiutendaji," amesisitiza Bw. Nyaisa.

Hata hivyo katika kusisitiza hayo ametoa mwelekeo wa taasisi kwa miaka ijayo, huku akigusia maboresho ya wa mfumo Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS) ambayo yatamwezesha mteja kujisajili kwa haraka zaidi na kuepuka kuwatumia vishoka.

Awali akitoa neno la utangulizi Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji Bw. Daimon Kisyombe ametoa wito kwa watumishi hao kuzingatia malengo na mpango mkakati wa taasisi ambao unalenga kufikisha huduma yenye tija kwa jamii na kuweka mazingira safi kwa wawekezaji nchini kupitia BRELA

 Katika hafla hiyo Bw. Nyaisa amewakabidhi watumishi hao vyeti vya ushiriki wa mafunzo ambavyo vimetolewa na Chuo cha Utumishi cha Umma Tanzania.

No comments:

Post a Comment