MSITUMIE VIJIWE KUPANGA VITENDO VYA KIHALIFU-MTAKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 15, 2022

MSITUMIE VIJIWE KUPANGA VITENDO VYA KIHALIFU-MTAKA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akizungungumza katika mkutano wa wenyeviti na makatibu wa vijiwe vya bodaboda na bajaji mkoani Dodoma leo Juni 15,2022

Mwenyekiti wa Umoja wa Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma, Keneth Chimoti akizungungumza katika mkutano wa wenyeviti na makatibu wa vijiwe vya bodaboda na bajaji mkoani Dodoma leo Juni 15,2022

Baadhi ya wenyeviti na makatibu wa vijiwe vya bodaboda na bajaji mkoani Dodoma leo Juni 15,2022 wakiwa katika mkutano wa kujadili mambo mbalimbali ikiwemo kuhamasishana katika kutenda matendo mema

Bilson Vedastus-Dodoma

Waendesha bodaboda na bajaji mkoani Dodoma wametakiwa kuacha kutumia vijiwe vyao vya bodaboda kama sehemu za kuchora ramani ili kupora watu, kubaka na kufanya vitendo vingine vya kihalifu na uvunjifu wa amani.

Onyo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka wakati akizungumza kwenye mkutano wake na wenyeviti na makatibu wa vijiwe vya bodaboda na bajaji mkoani Dodoma.

Pia ametumia mkutano huo kuwaalika waendesha boda na bajaji wote mkoani Dodoma wapatao 9,000 kufika katika mkutano utakaofanyika Jumapili ijayo ambao utatumika kujadili na kutafuta njia bora za kuondoa kero na kutafuta suluhisho la malalamiko yao na taasisi zinazosimamia usalama barabarani.

Mtaka amesisitiza kwamba, wale wote ambao wanajihusisha na vitendo vya kihalifu kwenye vijiwe vyao, wakibainika vyombo vya ulinzi na Usalama vitawachukulia hatua kali.

Amesema kama wapo waendesha bodaboda na bajaji ambao wanatumika katika kutenda vitendo hivyo vya kihalifu, wanatakiwa wawaambie wanaowatuma kwamba hawapo tayari kuendelea kutumika.

Mtaka amesema katika mkutano wake wa Jumapili pia atataja majina ya watu walioathiriwa na vitendo viovu vya kubakwa, kuibiwa na hata kuporwa mali mbalimbali.

Amesema, bodaboda na bajaji wa mkoa wa Dodoma wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuheshimu kazi zao na kwamba matazamio ya mkoa ni kuona kwamba wanakua na baadaye wanamiliki vyombo vikubwa kuliko kubaki deiwaka kwa miaka 10.

Ameahidi kwamba katika mkutano wa Jumapili atawakutanisha boda boda na bajaji zikiwemo taasisi za kifedha, bima na mfuko wa hifadhi za jamii (NSSF) ili kuwapa nafasi kujiunga na huduma hizo muhimu.

Mtaka amesema mkutano huo wa Jumapili unalenga kufungua ukurasa mpya wa uhusiano baina yao na watendaji barabarani ambao wamekuwa wakiwalamikia kwamba wanawanyanyasa.

Katika kurudisha uhusiano mzuri na taasisi hizo amesema, katika mkutano huo pia ataalika viongozi wa Jiji, Tarura na Polisi ili kutafuta suluhu ya malalamiko yao.

Pia atazialika taasisi mbalimbali ikiwemo Chuo chaTeknojia cha Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wataalamu wa CTI wa Chuo cha Biashara (CBE) na Chuo cha Mtakatifu Yohane ili kuonesha mifumo yao ya namna a kifuatilia nyendo za bodaboda na bajaji.

Mtaka pia ameahidi kuzialika kampuni zinazouza bodaboda na bajaji mkoani humo kama Kazimoto na City Boys na nyingine kueleza namna gani zinahusiana na kukubaliana na waendesha bodaboda na bajaji.

Mtaka amesema Jumapili hiyo itakuwa Siku ya Bodaboda na Bajaji katika mkoa huo pamoja na kutafuta suluhu za changamoto zao pia watapata chakula, nyama choma na burudani.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma, Keneth Chimoti amewataka viongozi wa bodaboda na bajaji kwenda kuhamasisha wenzao na kutoa kushirikiano ili kufanikisha mkutano huo wa Jumapili.

Chimoti amesema wanatakiwa kuwahamasisha ili wakutane na viongozi hao kwani lengo lao ni kisajiliwa na kujulikana wanafanya kazi katika vituo gani.

Amesema mkutano huo utakuwa mwanzo wa mabadiliko yao kwani utasaidia kukutana na taasisi za kifedha, vyombo vya ulinzi na usalama watendaji ili kumaliza kero za barabarani

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amesema katika kujenga mfumo wa kufuatilia upotevu wa boda inatakiwa kusajili na kuhuisha vituo vya boda boda.

Akitambulisha mfumo wa kufuatilia bodaboda Mhadhiri wa Chuo cha DIT, Budoya Christian amesema mfumo huo utasaidia kifuatilia upotevu na usalama wa waendeshaji.

No comments:

Post a Comment