Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau wote wa haki za watoto katika kuadhimisha “Siku ya Mtoto wa Afrika.” Siku hii inaikumbusha dunia juu ya mauaji ya watoto wapatao 2,000 wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini, waliouawa kikatili na iliyokuwa Serikali ya Makaburu.
Wakati tunaadhimisha siku hii muhimu wadau wote wa haki za watoto ni vyema kujitathmini namna tunavyolinda, kutetea na kuhifadhi haki za mtoto kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu inayosema: “Tuimarishe Ulinzi wa Mtoto: Tokomeza Ukatili Dhidi yake, Jiandae Kuhesabiwa.”
THBUB inatambua na kupongeza jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kulinda na kukuza haki za mtoto ikiwemo kuanzisha madawati ya Jinsia na Watoto katika Vituo vya Polisi, upatikanaji wa huduma ya afya kwa mama na mtoto, kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia mashauri ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto Zanzibar, kuwarejesha watoto wa kike waliopata ujauzito katika mifumo ya elimu, kuanzisha kamati za ulinzi wa mtoto nchini na kukemea ukatili wa kijinsia kwa watoto.
THBUB kwa upande wake imeendelea kutoa elimu kuhusu haki za watoto kupitia matamasha ya watoto na vilabu vya haki za binadamu na utawala bora ilivyoanzisha kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu. Pia, imeendelea kuhamasisha jamii kujiepusha na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kupitia vipindi vya radio, TV, semina, na maadhimisho.
Hata hivyo, pamoja na jitihada hizi bado kumekuwepo na changamoto kadhaa, ikiwemo: Watoto kuendelea kufanyiwa ukatili wa kingono, kupigwa, kutelekezwa na kuuawa; uelewa mdogo kwa wananchi kuhusu haki za mtoto; wananchi kumaliza mashauri ya jinai yanayowahusu watoto kifamilia; wananchi kutotoa taarifa juu ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto; na uwepo wa mila zenye madhara kwa watoto katika maeneo mbalimbali nchini.
Kutokana na changamoto zinazoathiri haki za watoto, THBUB inapendekeza yafuatayo:
1. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iendelee kutoa elimu kuhusu haki za watoto na athari za ukatili dhidi yao;
2. Viongozi wa dini waendelee kutoa elimu ya kiroho kwa wananchi ili kujiepusha na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto;
3. Wadau wa haki za binadamu waendelee kutoa elimu ya haki za binadamu kwa jamii ili kubadili mila na tamaduni potofu;
4. Vyombo vya kusimamia sheria vichukue hatua madhubuti dhidi ya watuhumiwa wanaojihusisha na vitendo vya ukatili;
5. Wazazi wawajibike katika kuwapa watoto malezi bora yenye kuzingatia maadili na desturi za kitanzania na kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji;
6. Wananchi watoe taarifa juu ya matukio yote ya ukatili na udhalilishaji dhidi ya watoto; na
7. Wadau wote wa haki za watoto waendelee kushirikiana katika kulinda, kuhifadhi na kukuza haki za watoto.
THBUB inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali, wananchi na wadau mbalimbali katika kulinda, kuhifadhi na kukuza haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Imetolewa na:
(SIGNED)
Mohamed Khamis Hamad
Makamu Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
No comments:
Post a Comment