WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA SLOVAKIA AWASILI NCHINi KWA ZIARA YA KIKAZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 10, 2026

WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA SLOVAKIA AWASILI NCHINi KWA ZIARA YA KIKAZI


Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Ulaya wa Jamhuri ya Slovakia, Mhe. Juraj BlanĂ¡r, amewasili nchini kwa ziara ya kikazi kuanzia Juni 10 hadi 11, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Slovakia.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam Mhe. Juraj BlanĂ¡r alilakiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. James Milya (Mb).

Akiwa nchini, Mhe. BlanĂ¡r atashiriki katika mazungumzo ya pande mbili na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) yatakayofanyika Juni 11 2026.

Ziara hii inalenga kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, elimu, programu za ufadhili wa masomo, usalama wa mtandao, biashara na uwekezaji.

Baada ya mazungumzo na mwenyeji wake watazungumza na waandishi wa habari na baadaye watashiriki katika hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Slovakia jijini Dar es Salaam. Ubalozi huo ulifunguliwa mwezi Novemba 2025 na unaashiria dhamira ya pamoja ya Tanzania na Slovakia ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia pamoja na kupanua maeneo ya ushirikiano wa maendeleo na uchumi.

Waziri BlanĂ¡r ambaye ameambatana na wafanyabiashara wapatao 50 atashiriki katika Kongamano la Biashara la Tanzania Slovakia litakalokutanisha wafanyabiashara na wawakilishi wa sekta binafsi kutoka nchi zote mbili.

Kongamano hilo linatarajiwa kujadili fursa za biashara na uwekezaji, kukuza uhamishaji wa teknolojia na kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati zikiwemo nishati jadidifu, uchakataji wa mazao ya kilimo na ubunifu wa kidijitali.

No comments:

Post a Comment