Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Kauli hiyo imetolewa Juni 10,2026 na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati akizindua ghala la kwanza la forodha katika Mkoa wa Dodoma linalomilikiwa na Kampuni ya Ciwaye Trading Company Limited, wilayani Chamwino.
Dkt. Mwigulu amesema sekta binafsi ni mhimili muhimu wa uchumi wa taifa na kwamba maendeleo ya nchi hayawezi kufikiwa bila ushiriki mkubwa wa wawekezaji wa ndani na nje.
“Kama tunavyoheshimu sekta ya umma, tunapaswa pia kuheshimu sekta binafsi kwa uzito ule ule kwa sababu ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi katika mataifa mengi yaliyoendelea,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho ya sheria za uwekezaji ili kuongeza ushiriki wa wazawa katika shughuli za kiuchumi na kuhakikisha wanapata manufaa ya vivutio vya uwekezaji vinavyotolewa nchini.
Dkt. Mwigulu amesema hatua nyingine iliyochukuliwa ni kuondolewa kwa zaidi ya tozo 270 zilizokuwa kero kwa wafanyabiashara na walaji, hatua ambayo imechangia kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Akizungumzia mradi huo, amesema uwekezaji wa ghala la forodha una umuhimu mkubwa katika kuongeza ufanisi wa biashara, mapato ya Serikali na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Ukubwa wa mradi huu haupimwi kwa majengo yake, bali kwa matokeo yake katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050,” amesema.
Pia amewataka wakuu wa mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kuendelea kuboresha miundombinu na kuweka mazingira rafiki yatakayovutia uwekezaji zaidi katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ciwaye Trading Company Limited, Happy Niclas John, amesema mradi huo uliogharimu zaidi ya Sh bilioni tatu umekamilika kwa asilimia 100 na unatarajiwa kuongeza fursa za biashara na ajira kwa wananchi.
Amesema kampuni hiyo itahakikisha shughuli zote za ghala zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vinavyotakiwa ili kutoa huduma bora kwa wateja.
Naye Mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wahab Matengo, amesema maghala ya forodha yana mchango mkubwa katika kurahisisha biashara ya kimataifa, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kukuza ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uchumi wa nchi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika biashara za kikanda na kimataifa.







No comments:
Post a Comment