Na Mwandishi wetu Iramba
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kufikisha huduma mbalimbali za jamii zikiwemo za afya kwa wananchi wote hadi waishio maeneo ya vijijini ili wazipate kwa wakati.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Julai 16, 2022) wakati akizungumza na wananchi katika kata ya Mtoa wilayani Iramba baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha afya cha Mtoa akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Singida.
Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutawawezesha wananchi hao kupata huduma za afya zikiwemo za maabara, mama na mtoto na upasuaji karibu na makazi yao. “Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza huduma za afya ziwafikie wananchi wote hadi waishio vijijini.”
Waziri Mkuu amesema kwa wilaya ya Iramba, Serikali imeidhinisha shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya sita kwa lengo la kusogeza huduma hizo karibu na makazi ya wananchi.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameupongeza uongozi wa wilaya ya Iramba kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa kituo cha afya cha Mtoa, ambapo ameiagiza Wizara ya Fedha ya Mipango kupeleka kiasi cha shilingi milioni 262, 635,689 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.



No comments:
Post a Comment