MUHIMBILI MBIONI KUANZA UPANDIKIZAJI INI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, July 29, 2022

MUHIMBILI MBIONI KUANZA UPANDIKIZAJI INI

Mkurugenzi wa Tiba Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Hedwiga Swai akizungumza wakati wa ufunguzi wa zoezi la upimaji wa homa ya ini bila malipo, lililofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Idara ya Magonjwa ya ndani.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. John Rwegasha akizungumza wakati wa ufunguzi wa zoezi la upimaji wa homa ya ini bila malipo, lililofanywa na Hospitali ya Taifa.
Zoezi la upimaji wa homa ya ini likiendelea
Baadhi ya wananchi waliohudhuria katika zoezi hilo la upimaji wa homa ya ini
Baadhi ya wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Na Angel Mndolwa Dar-es-salaam

Hospitali ya Taifa Muhimbili imeanza maandalizi ya kupandikiza Ini ikiwa ni mikakati ya kukabiliana na tatizo la homa ya ini ambayo inakadiriwa kusababisha vifo vya watu milioni moja kila mwaka duniani.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Tiba Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Hedwiga Swai wakati wa ufunguzi wa zoezi la kupimaji wa homa ya ini bila malipo, lililofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Idara ya Magonjwa ya ndani katika kuadhimisha siku ya ini duniani inayoadhimishwa Julai 28 kila mwaka.

Dkt. Swai amesema kuwa tayari hospitali imeanza michakato ya kusomesha wataalamu na kuboresha miundombinu ikiwa ni maandalizi ya kuanza kupandikiza ini ambayo ndio tiba kamili kwa watu wenye magonjwa hayo ambao matibabu mengine yameshindikana.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani za mwaka 2021 Tanzania kuna vifo takribani 1400 vinavyosababishwa na tatizo la ini hususani aina B (Hepatitis B) na kila baada ya sekunde 30 anafariki mtu mmoja duniani kutokana na tatizo la homa ya ini.

“Hospitali ya Taifa Muhimbili imejikita katika mapambano dhidi ya tatizo hili kwa kuendelea kuwapokea na kuwapa huduma mbalimbali wagonjwa wa wanaoletwa kwa uchunguzi au matibabu ya ini, tumeanzisha kliniki ya magonjwa ya Ini mbayo hufanyika kila jumatatu” amesema Dkt. Swai

Kuhusu dalili za ugonjwa wa homa Dkt. Swai amesema kwamba zinafanana sana na magonjwa mengine ya kawaida hii inapelekea watu kudharau kufanya uchunguzi mapema jambo linalopelekea ugonjwa kukua na kufikia mgonjwa kuanza kutapika damu, mwili kuwa wa njano na tumbo kujaa maji.

Dkt. Swai ametoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kupima na kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara kwa kuwa ugonjwa unapogundulika katika hatua za awali ni rahisi kuutibu na kupunguza maradha yake ambayo ni pamoja na saratani ya ini.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. John Rwegasha alitaja kuwa mbali na homa ya ini kusababishwa na virusi A, B, C, D na E, lakini unywaji wa pombe kupita kiasi unatajwa miongoni mwa sababu.

Mmoja wa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Jonathan Nangwa, ambaye ni mmoja wapo kati ya wananchi waliojitokeza kupimwa ini, ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kufanikisha zoezi hilo bila malipo kwa kuwa limetoa fursa ya watu hata ya kipato cha chini kushiriki.

Jumla ya wananchi 275 waliojitokeza kufanya uchunguzi wa homa ya ini , 13 kati yao walibainika kuwa na maambukizi, na tayari wameeingizwa katika mfumo wa matibabu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

No comments:

Post a Comment