Rais Samia ameibeba Sekta ya Kilimo- Katibu Tawala Manyara - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 26, 2022

Rais Samia ameibeba Sekta ya Kilimo- Katibu Tawala Manyara

Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Karolina Mthapula akizungumza na washiriki wa mafunzo ya mfumo wa mbolea ya ruzuku yanayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Babati tarehe 25 Agosti, 2022.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Kaskazini, Gothard Liampawe akiendelea na mafunzo ya mfumo wa mbolea za ruzuku kwa wadau wakioshiriki mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Babati tarehe 25 Agosti, 2022
Gothard Liampawe Kaimu Meneja TFRA kanda ya Kaskazini (aliyesimama) akiendelea na mafunzo ya namna mfumo wa mbolea ya ruzuku unavyofanya kazi ili Wakuu wa Idara za Kilimo Umwagiliaji na Ushirika wa halmashauri za mkoa wa Manyara waweze kuumiliki na kupandisha majina ya wakulima waliosajiliwa kwenye vitabu vilivyosambazwa vijiji vyote nchini. Ni katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara
Wakuu wa Idara za Kilimo Umwagiliaji na Ushirika wa halmashauri za mkoa wa Manyara wakifurahia baada ya kuulewa mfumo wa mbolea za ruzuku baada ya mafunzo yaliyotolewa na Kaimu Meneja wa TFRA kanda ya Kaskazini Gothard Liampawe (aliyesimama) katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Babati mji mkoani Manyara tarehe 25 Agosti, 2022
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Karolina Mthapula (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha na wataalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) walipofika ofisini kwake kueleza ùmuhimu wa mafunzo ya mfumo wa mbolea za ruzuku kwa wadau wa mbolea mkoani hapo.

Na Mwandishi wetu- Manyara 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Karolina Mthapula ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuamua kuibeba Sekta ya Kilimo na kutenga kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 150 kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima na kuwapunguzia mzigo wa bei.

Ametoa shukrani hizo mara baada ya wataalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kufika mkoani hapo na kufanya mafunzo ya namna mfumo wa mbolea ya ruzuku unavyofanya kazi kwa Maafisa ugani, waingizaji na mawakala wa mbolea wa mkoa huo.

“Mama Samia ameamua kuibeba hii sekta, watanzania wengi wamejiajiri kwenye kilimo na ili kuongeza tija kwenye kilimo chao na taifa kwa ujumla ni lazima kutumia mbolea na kilimo kifuate taratibu zote za kilimo bora” aliongeza Karolina.

Aidha, Kalorina aliitaka TFRA kwa kushirikiana na maafisa ugani nchini kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima ili kuwaongezea uelewa na kuondoa dhana potofu ya kuwa mbolea za viwandani zina madhara kwenye ardhi na afya za walaji.

Kwa Upande wake, Faraja Ngeregeza Katibu Tawala Msaidizi wa masuala ya Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Manyara alitoa wito kwa wakulima kwenda kujisajili ili waweze kunufaika na mbolea za ruzuku zinazotolewa na serikali sikivu ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Pia amewataka washiriki kusikiliza kwa makini maelekezo yanayotolewa katika mafunzo hayo ili kwenda kuwa mabalozi kwa wale walioshindwa kuhudhuria mafunzo hayo ili kwa pamoja wasimamie na kutekeleza mpango wa serikali wa mbolea za ruzuku kwa ufanisi.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wengine, mkulima Hussein Rajab ameishukuru serikali kwa kuja na mpango wa ruzukuna kubainisha umewapunguzia mzigo mkubwa wa kugharamia mbolea na kueleza mwaka huu watalima kwa wingi Zaidi maana wamewezeshwa

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TFRA kanda ya Kaskazini, Gothard Liampawe alieleza lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha mpango wa ruzuku unatekelezwa kwa ufanisi kama serikali ilivyoelekeza huku ikiondoa mianya ya udanganyifu iliyoweza kujitokeza kwenye ruzuku zilizotolewa miaka ya nyuma.

Aliongeza kuwa mafunzo pamoja na usajili wa wakulima ni endelevu na kutoa wito wakati wowote mafunzo yanapoandaliwa wasisite kujitokeza ili kuwa na uelewa wa pamoja katika kusimamia tasnia ya mbolea nchini.

Baada ya mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Babati tarehe 25 Agosti, 2022, yalichukua takribani masaa matatu ambapo washiriki waliweza kujionea namna mfumo unavyofanya kazi kwa kuuza mbolea kupitia kampuni la ETG Input ya mkoani Babati.

No comments:

Post a Comment