Ni kauli ya Neville Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), wakati akizungumza kwenye kipindi cha Pambazuko kinachorushwa na Kituo cha Radio cha MVIWATA (MVIWATA FM), mjini Morogoro hii leo Agosti 30,2022.
“Baada ya malalamiko ya wadau wa habari, serikali ya awamu hii (Awamu ya Sita) ilisikia na ndio iliyoanza kuleta mapendekezo ya mabadiliko ya sheria. Kwenye mapendekezo hayo, ilianza katika kipengele cha 38.
“Sasa mapendekezo hayo yalipotufikia sisi wadau wa habari, tulikaa kwa pamoja na tukasema tuanze na kipengele cha kwanza. Na kwa kuwa ilikuwa na dhamira ya kweli ya kupitia mabadiliko ya vipengele hivyo, tayari kikao cha kwanza cha wadau na serikali kimeishafanyika,” amesema Meena.
Katika kipindi hicho Meena amesema, serikali ilianza kuonesha dhamira ya dhati tangu pale Rais Samia Suluhu Hassan alipokaa kikao na wanahabari Ikulu, Dar es Salaam.
“Si hivyo tu, bado Rais Samia aliagiza kufunguliwa kwa televisheni za mtandao zilizokuwa zimefungiwa, na zaidi katika serikali yake hiyo hiyo magazeti yaliyokuwa yamefungwa kipindi kirefu nayo yalifunguliwa.
“Yote haya yanaonesha kwamba, suala la serikali kutaka kumaliza malalamiko ya wadau wa habari nchini lipo wazi, na sisi tunatumia wakati huu kuhakikisha tunafikia malengo,” amesema Meena.
Akizungumzia mapokeo ya Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 baada ya kusainiwa na kuwa sheria, Meena amesema sheria hiyo ndani ya saa 24 ilianza kupingwa na wadau
“Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipingwa na wadau wa habari siku moja baada ya kupitishwa ili kutumikaa. Si kwamba, hakukuwa na vitu muhimu kwa wanahabari, wadau waliona imebeba mitego na madhara mengi kwa wanahabari na vyombo vya habari,’’ amesema Meena.
Akizungumza kwenye Radio hiyo amesema, kutokana na yaliyomo kwenye sheria hiyo, wadau wa habari waliamini vyombo vya habari vitazidi kuharibika.
‘‘Wadau wa habari wakiwemo Jamii Forym, TAMWA, UTPC, MCT, MISA-TAN, LHRC, TLS, Twawezaa, Sikika, THRDC na wengine, walikaa pamoja na kuangalia madhara yanayoweza kutokea kutokana na sheria hiyo.
‘‘Tunashukuru hatua zilipofika kwa sasa. Rais (Ramia Suluhu Hassan) amekuwa na utashi wa kufanya mabadiliko lakini hata waziri aliyepo sasa (Nape Nnauye), mwelekeo wake ni huo,’’ amesema Meena.
No comments:
Post a Comment