UPATIKANAJI WA MAJISAFI KWA WAKAZI NDANI YA ENEO LETU LA HUDUMA NI ASILIMIA 96 -DAWASA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, August 13, 2022

UPATIKANAJI WA MAJISAFI KWA WAKAZI NDANI YA ENEO LETU LA HUDUMA NI ASILIMIA 96 -DAWASA

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja,akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 13,2022 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2022-2023.

Na Okuly Julius-Dodoma

Mamlaka ya Majisafi Na Usafi wa mazingira Dar-es-salaam (DAWASA) imefanikiwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za majisafi Kwa wakazi ndani ya eneo lake zaidi ya asilimia 96 kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na miradi midogo ya kusogeza mtandao wa Maji kwa wananchi

Hayo yamesemwa leo Agosti 13,2022 na Afisa mtendaji mkuu wa Dawasa Eng.Cyprian Luhemeja wakati akizungumza Na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa bajeti ya mwaka 2022-2023.

Aidha, Eng.Luhemeja amesema kuwa sehemu kubwa ya eneo linalohudumiwa Na DAWASA linapata huduma ya maji ya uhakika baada ya miradi ya kimkakati kukamilishwa ikiwemo upanuzi wa mitambo ya Ruvu Juu Na Ruvu chini,ulazaji wa mabomba makubwa na madogo na ujenzi wa matenki ya kuhifadhia maji na hii kupelekea idadi ya wateja kuongezeka kutoka wateja 217,766 mwaka 2018 hadi kufikia wateja 370,982 mwaka huu 2022.

"Nataka niwaambie tu kuwa kwa mwaka wa fedha tuliounza hivi karibuni wa 2022/2023 tunatekeleza miradi 13 ya majisafi na usafi wa mazingira yenye thamani ya shilingi zipatazo Trilioni 1.029 na kwa miradi hiyo ikikamilika tutafikia asilimia miamoja"Amesema Eng.Luhemeja

Eng.Luhemeja ametaja Miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa uboreshaji wa mfumo wa usambazaji maji kuanzia Chuo kikuu cha Ardhi hadi Bagamoyo ,miradi ya maji Mshikamamo ,mradi wa Maji Kigamboni, mradi wa Maji Chalinze awamu ya tatu, mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda, miradi ya maji safi ya pembezoni,mradi wa kupunguza kiwango cha maji yasiyolipiwa,mradi wa Uboreshaji wa Ufanisi wa Utendaji (PIP).

Miradi mingine ni ile ya ujenzi wa mtambo wa majitaka Mbezi Beach ,mradi wa ujenzi wa mtambo wa majitaka Buguruni ,mradi wa uboreshaji wa mifumo ya majitaka pembezoni ,mradi wa ujenzi wa vituo vya huduma za usafi kwa umma (Public Sanitary Service Points) pamoja na ununuzi wa magari ya majitaka

Pia Eng.Luhemeja amesema kuwa Maeneo yatakayopata maji kwa uwiano mzuri baada ya miradi mikubwa kukamilika ni pamoja na Wilaya nzima ya Kigamboni, Vikawe, Kimele, Goba Adora , Goba kwa Awadhi, Bwawani, Mivumoni, Madale, Mbezi Juu, Goba Usukumani hadi Power Nyati, Mbezi Mshikamano, Bonde la Mpunga, Tegeta A na Mbezi Luis.

Maeneo mengine ni pamoja na Mbagala Kibondemaji, Toangoma, Mbande, Kigamboni, Mwandege, Zingiziwa na maeneo ya Mkuranga kati ya Kiguza na Vikindu.

Afisa Mtendaji huyo amebainisha kuwa uhakika wa upatikanaji wa Maji katika eneo la huduma la DAWASA Ili kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji katika eneo la huduma la DAWASA litakaloendana na ongezeko ya idadi ya watu na matumizi ya shughuli za maendeleo ikiwemo Viwanda, miradi mikubwa miwili inatarajiwa kuanza kutekelezwa ndani ya mwaka wa fedha 2022/23.

Eng.Luhemeja amesetaja miradi hiyo kuwa ni Miradi ya ujenzi wa bwawa la Kidunda kuhakikisha maji yanapatikana mwaka mzima katika mto Ruvu na ujenzi wa Mtambo mkubwa wa uzalishaji maji katika mto Rufiji,mradi wa Rufiji unatarajiwa kuzalisha lita milioni 750 za maji kwa siku na hivyo uzalishaji maji utaongezeka mara dufu na hivyo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji ambayo ni muhimu kwa uhai na maendeleo ya kiuchumi.

Ikumbukwe tu kuwa kwa sasa DAWASA inategemea vyanzo vikuu vya maji vinne ambavyo ni Mto Ruvu, Mto Wami, Mto Kizinga na visima virefu.

No comments:

Post a Comment