Na Mwandishi wetu Morogoro
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Posta Tanzania, Brigedia Jenerali Mstaafu Yohana Mabongo amewataka Viongozi wa Shirika la Posta nchini kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Ameyasema hayo tarehe 05 Agosti, 2022 wakati alipokuwa akifunga rasmi Kikao Kazi cha Viongozi hao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza wa Chuo Kikuu SUA, mjini Mororgoro.
Akizungumza wakati akifunga kikao hicho Brigedia Generali Mstaafu Mabongo amewataka Viongozi hao kuwajibika kila mmoja katika nafasi yake huku akitoa wito kwa Viongozi hao kubadilisha mitazamo yao Ili kufanya kazi kwa Ubunifu wakati wa kutimiza majukumu yao ili kuendelea kutoa huduma zinazoendana na mahitaji ya wananchi.
Aidha, Mwenyekiti Mabongo amesisitiza kikao hicho kiwe chachu ya kuhakikisha kila kiongozi anatoka na mabadiliko yatakayoongeza ufanisi katika eneo lake la kazi, kubuni mbinu mpya za kiutendaji pamoja na kufanya tathmini ya utendaji wao ili kuongeza tija kwa Shirika.
“Niwatake nyote baada ya kutoka hapa, mkakae na kufanya tathmini na wafanyakazi wenu kila mmoja kwenye eneo lake hii itasaidia kuchukua hatua stahiki za maboresho ili matarajio ya Serikali yaweze kufikiwa”. Amesema Mwenyekiti Mabongo.
Sambamba na hilo Brigedia Generali Mstaafu Mabongo ametumia nafasi hiyo kumpongeza Postamasta Mkuu pamoja na Menejimenti ya Shirika la Posta Tanzania kwa juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanywa katika mageuzi ya Shirika yenye lengo la kuboresha huduma zinazotolewa ili ziwafikie wananchi wengi zaidi na zikidhi mahitaji yao halisi.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti Mabongo, amekabidhi zawadi kwa mikoa mitatu iliyofanya vizuri katika utendaji, mikoa hiyo ni Lindi (1), Morogoro (2) na Mara (3) mikoa hii iliweza kutimiza vigezo vyote vitatu vya upimo.
Vilevile alikabidhi zawadi kwa kiongozi hodari kwa upande wa Mameneja mikoa (Joyce Chirangi-Mara) na Eric Maximillian (Makao Makuu).
Kwa upande wake Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbodo, amemshukuru Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo kwa kufika na kufunga kikao kazi hicho na kuahidi kuwa, watazingatia maelekezo yote kwa niaba ya Menejimenti yake pamoja na wafanyakazi kwa maslahi mapana ya Shirika na umma wa watanzania kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment