Na Okuly Julius-Dodoma
KAMATI ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, imesema kuwa thamani ya Fedha ya shilingi bilioni 3.8 iliyotumika katika ujenzi wa makao makuu ya Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) imeonekana.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 8 Septemba 2022 na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe Stanslaus Nyongo (Mb) wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa Ofisi za Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) Jijini Dodoma.
Mwenyekiti Nyongo amesema kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inastahili pongezi kubwa kwa kutafrisi kwa vitendo maelekezo ya serikali kuhamia Dodoma kwa kuhamishia ofisi zake na taasisi zilizopo chini yake.
Mhe Nyongo amesema kuwa kujengwa kwa ofisi na kuhamia Jijini Dodoma kutarahisisha wananchi kupata huduma kwa urahisi na ukaribu kwani huduma hiyo ni muhimu kwa Usalama wao na usalama wa Taifa kwa ujumla.
“Sisi kama kamati tumeridhika kwa kuja na kuona na tunaahidi tutakuja tena kujionea kazi zinazofanywa pindi jengo litakapoanza kutumika” Amekaririwa Mhe Nyongo
Mwenyekiti huyo ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha kuwa inawatangazia wananchi kwa kila hali ili waweze kujua kuwa huduma zimerahisishwa na tayari zinapatikana makao makuu ya nchi.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amesema kuwa ziara hiyo ya kamati ya Bunge kuangalia ujenzi wa ofisi za kitaifa za Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) imefikia hatua nzuri za ujenzi na hiyo ni sehemu muhimu katika utekelezaji wa maelekezo ya serikali kuhamia Jijini Dodoma.
Waziri Mkenda amesema kuwa utekelezaji huo wa maelekezo ya serikali unaenda sambamba na ujenzi wa majengo ya Taasisi za Wizara ili wafanyakazi wanapohamia Dodoma wawe na sehemu ya kufanyia kazi na Taasisi isikodi sehemu ya kuafanyia kazi.
Kadhalika amempongeza Mtendaji Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomoki Prof Lazaro kwa utekelezaji mzuri wa ujenzi wa Ofisi Jijini Dodoma ambao umefikia asilimia 85
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Prof.Lazaro Busagala, amesema kuwa ujenzi huo unahusisha maabara na ofisi za taasisi hiyo pindi itakapohamisha makao yake Dodoma.
Amesema kuniliki ofisi itasaidia kuounguza gharama za kupangisha ofisi hivyo kuokoa fedha nyingi za serikali ambazo zingetumika katika upangishaji wa ofisi.



No comments:
Post a Comment