Na. Sifa Stanley, DODOMA
MKUU wa Divisheni ya Elimu Sekondari Jiji la Dodoma Upendo Rweyemamu, ameagiza shule zote za Jiji la Dodoma kuendesha midahalo ndani ya shule kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi kujifunza lugha ya kiingereza ili wafanye vizuri katika masomo yao.
Ametoa agizo hilo katika hafla ya kufunga mashindano ya mdahalo ya wanafunzi wa shule za sekondari za jiji la Dodoma iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Dodoma.
Mkuu huyo amesema kuwa ni muda muafaka kwa shule za sekondari zilizopo jiji la Dodoma kuanzisha utaratibu wa kuendesha midahalo ndani ya shule zao ili kuweza kuwasaidia wanafunzi kupata maarifa ya lugha ya kiingereza na kuwajengea hali ya kujiamini.
“Mdahalo huu tumeanza kwa ngazi ya Wilaya, lakini nimesisitiza wakati nazungumza na walimu pamoja na wanafunzi kwamba suala hili la mashindano ya midahalo liende ngazi ya shule pia, lifike hadi ngazi y darasa mfano kidato cha kwanza wanashindana na kidato cha tatu au kidato cha tano washindane na kidato cha nne. Kwakufanya hivi itasaidia kuwajengea ujuzi wa kuzungumza pamoja na kuandika lugha ya kiingereza ambayo ni lugha inayotumika kwa asilimia kubwa, lakini pia itawasaidia kufanya vizuri”, alisema Rweyemamu.
Akieleze umuhimu wa shindano la mdahalo uliofanyika kwa muda wa wiki mbili, alisema mdahalo huo unamchango mkubwa sana kwa shule za Jiji la Dodoma na utasaidia kuinua ufaulu wa wanafunzi wa shule za sekondari wa jiji hilo.
“Umuhimu wa huu mdahalo kwa shule zetu za sekondari ni kwamba lugha tunayotumia kufundishia ni lugha ya kiingereza isipokuwa kwenye masomo ya lugha kama vile Kiswahili ,kiarabu na kichina, hii siku ya leo ni muhimu kwasababu tunaenda kuongeza ufaulu wa watoto wetu kwasababu watakuwa vizuri kwenye lugha hii inayotumika kufundishisha masomo yao shuleni”, amesema Rweyemamu.
Naye, Mratibu wa shindano la mdahalo Masoud Malick, ameeleza lengo lakufanya shindano la mdahalo ni kuwasaidia wanafunzi kuwa na akili iliyochangamka na kuwajengea mazingira ya kufahamiana na wanafunzi wengine.
“Mashindano haya yana lengo mahususi la kuwasaidia wanafunzi kuchangamsha akili zao kwasababu wanakutana na wanafunzi kutoka shule mbalimbali na wenye uwezo tofauti, lakini pia yatasaidia kujenga uelewa wa masuala ya ukatili wa kijinsia na umuhimu wa utunzaji wa mazingira kutokana na mada walizozizungumzia katika mdahalo”,ameeleza Malick.
Kwa upande wake Pili Hamza mwanafunzi wa shule ya Sekondari Miyuji, alifafanua namna alivyonufaika na mashindano ya mdahalo “haya mashindano yanatusaidia sana kwa kuweza kujieleza, lakini pia kujijengea ujasiri wa kuweza kueleza maovu yanayoendelea katika jamii kwasababu tunaweza kusimama mbele za watu na kujieleza” amesema Hamza.
Ikumbukwe kuwa mashindano ya mdahalo ya shule za sekondari za jiji la Dodoma yalianza rasmi Oktoba 1 2022, yakiwa na jumla ya Shule 16 zilizoshiriki shindano hilo, na yalifikia tamati Oktoba 10 2022, na Shule ya Sekondari Miyuji iliibuka kinara katika shindano hilo kwa kushika nafasi ya kwanza kati ya shule zote shiriki.



No comments:
Post a Comment