Na Immaculate Makilika MAELEZO, Ludewa
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amekagua vifaa vya ujenzi wa mnara wa mawasiliano utakaojengwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya Tigo katika Kijiji cha Nkwimbili Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe.
Ambapo baadhi ya vifaa alivyokagua ni pamoja na nondo, taa za mnara, miguu ya mnara, jenereta, mtambo wa kudhibiti umeme na betri.
Akihutubia wananchi jana (Novemba 27, 2022) katika Kijiji cha Lupingu wilayani humo, Mhe. Naibu Waziri Kundo amesema kuwa lengo la kutembelea mradi huo ni kujua utakamilika lini na huduma watakazopata wananchi.
Ifikapo Januari 2023 mnara huu utaanza kutoa huduma kwa wananchi na hivyo kutatua changamoto ya mawasiliano katika eneo hili. Wizara tuna miradi ya mipakani na maeneo maalum ili kuhakikisha wananchi wanapata mawasiliano kutoka nchini kwanza ikiwa ni pamoja na kuchangia uchumi wa nchi kwa manufaa yetu sote, ameeleza Mhe. Naibu Waziri Kundo.
Hata hivyo amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wakati wa ujenzi wa mradi huo pamoja na kuulinda mara utakapoanza kutoa huduma, huku akiwasii kutumia vizuri fursa za mawasiliano watakazopata kutokana na mnara huo.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa mnara katika Kijiji cha Nkwimbili kutoka Kampuni ya GNC Solutions LTD, Bw. Suleiman Senga ameahidi kuwa mnara huo utaanza kutoa huduma ifikapo Januari 2023 na kuwa kampuni zingine za simu zinaweza kutumia mnara huyo wa Kampuni ya Tigo kutoa huduma kwa wananchi kupitia kampuni zao.
Kuhusu mnara wa TBC uliopo Milo wilayani humo, Mhe. Naibu Waziri Kundo amesema kuwa kupitia mnara huo vituo vya vingine vya redio vinaruhusiwa kuweka vifaa vyao ambavyo vitasaidia kuongeza usikivu wa matangazo yao.
Katika hatua nyingine, Mhe. Naibu Waziri Kundo ameielekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha kuwa wanazingatia utaratibu na kuzisaidia kupata leseni kwa haraka redio mbalimbali zilizowasilisha maombi yao ikiwa ni pamoja na redio za halmashauri.
No comments:
Post a Comment