SERIKALI ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China leo Novemba 27, 2022 zimesaini mikataba ya mashirikiano ya pamoja katika kuboresha huduma za afya nchini.
Hafla ya makubaliano hayo yameongozwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel na Makamu Waziri wa Afya wa Jamhuri ya watu wa China Mhe. CAO Xuetao katika Ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mollel amesema, mashirikiano hayo yamelenga katika maeneo ya kujenga uwezo katika eneo la watoto, kubadilishana teknolojia katika maeneo ya upasuaji wa mishipa (Neurosurgery), eneo la Saratani na upasuaji wa Moyo (Cardiology).
Amesema, lengo la jumla la kusaini mashirikiano hayo ni kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zote mbili utaoleta manufaa katika pande zote ili kukidhi uboreshaji wa matibabu na afya kupitia mafunzo kwa Wataalamu.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema mashirikiano hayo yatapunguza gharama kwa Serikali kwa kupunguza rufaa za nje ya nchi zisizo za lazima na kutumia rasilimali hizo katika kuboresha huduma nyingine nchini.
Aidha, Dkt. Mollel ameushukuru ujumbe huo kutoka Jamhuri ya watu wa China kwa tukio hilo na kuweka wazi kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuboresha huduma za afya nchini.
Kwa upande wake Makamu Waziri wa Afya wa Jamhuri ya watu wa China Mhe. CAO Xuetao amesema kuwa, China na Tanzania zimekuwa uhusiano wa karibu na kusaidiana katika maendeleo ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali.
Amesema China imekuwa ikileta wataalam wa afya kuja nchini kusaidia katika utoaji wa huduma za afya ambapo hadi sasa wameshatoa huduma kwa watu zaidi ya Milioni 25.
Mhe. Mr. CAO Xuetao amesema kupitia makubaliano hayo wataalam kutoka Tanzania wataongezewa ujuzi katika fani mbalimbali za afya ili kuweza kutoa huduma bora za afya hapa nchini.
No comments:
Post a Comment