Na Mwandishi wetu Mbeya
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Mamlaka zinazohusika na utunzaji wa vyanzo vya maji ,kuwateremsha wananchi walioko kwenye maeneo ya milima kote nchini ambayo ni vyanzo vya maji na kuweke mipaka ili kupanda miti ya asili kwenye vyanzo vya maji vilivyopo milimani na kwenye maeneo oevu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya upandaji miti rafiki kwa vyanzo vya maji,iliyofanyika leo Novemba 16,2022 Jijini Mbeya Dkt.Mpango ameitaka TFS kama kuna miti ambayo ni rafiki wa maji waongeze juhudi katika kila Mkoa kutambua miti yote ya aina hiyo na kuiandalia vitalu ili iwe na miche ya kutosha.
"Naagiza Mamlaka husika na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwateremsha walioko kwenye maeneo ya milima kote nchini ambayo ni vyanzo vya maji ili tulinusuru Taifa letu, tuweke mipaka ili tupande miti ya asili kwenye vyanzo vya maji vilivyopo milimani na kwenye maeneo oevu,
Na kuongeza kuwa "Kampeni ya upandaji miti tuliyoianzisha leo ambayo itafanyika nchi nzima kwenye vyanzo vyetu vya maji, niwahakikishie kuwa ni jambo muhimu kwa uhai na usalama wa Watanzania,"Amesema Dkt.Mpango
Dkt.Mpango ametoa rai kwa Watanzania kubadilika na kuanza kutunza na kulinda vyanzo vyote vya maji ili nayo yawatunze, na kuungana na viongozi wengine kuangalia tena utaratibu wa kutunza vyanzo vya maji.
"Wote tunapenda biashara lakini isiwe biashara ambayo inaondoa uendelevu wa vyanzo vya maji, naomba tuelewane kuwa tuliyonayo sasa ni vita na kama Taifa lazima tuishinde, tukizembea uhaba wa maji utakuwa mkubwa zaidi,"Amesema Dkt.Mpango
Pia Dkt.Mpango amewataka wafugaji, wakulima na wenye viwanda kuhakikisha matumizi ya rasilimali maji wanayafanya kwa namna ambayo ni endelevu, na kuepuka kuchafua vyanzo vyetu vya maji.
Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mhe. Dkt. Tulia Ackson
amesema kuwa Chanzo cha maji Nzovwe kilichopo mkoani Mbeya kinatunzwa na wadau wengi, kipekee amewashukuru Machifu kwani nao wanaongoza vizuri kwenye utunzaji wa vyanzo vya maji.
"Nawashukuru na kuwapongeza TFS kwa kupanda miti lakini natamani ule upandaji miti utazame zaidi kwenye upande wa utunzaji mazingira kuliko kuwa miti ya kibiashara kwa sababu ikifika kipindi lazima ikatwe,"Dkt.Tulia
No comments:
Post a Comment