WIZARA YA ELIMU ZANZIBAR YAKABIDHIWA JUMLA YA VISHKWAMBI 6,600 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, December 22, 2022

WIZARA YA ELIMU ZANZIBAR YAKABIDHIWA JUMLA YA VISHKWAMBI 6,600




NA WyEST,DAR ES SALAAM

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia leo Desemba 22, 2022 imetoa jumla ya vishkwambi 6,600 kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa ajili ya kugawa kwa walimu ili kuwapa motisha na kuvitumia kama vitendea kazi.

Makabidhiano hayo yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam kati ya Dkt. Francis Michael, Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na  Khamis Abdulla Said, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi na maafisa wa Wizara hizo.


Katika hafla hiyo Dkt. Michael amesema Kati ya vishkwambi 300,000 vilivyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya zoezi la Sensa ya watu na makazi iliamriwa vigawiwe katika sekta ya elimu ambapo vishkwambi 6,600 ni kwa ajili ya walimu Zanzibar.

"Huku Bara tuliwapa walimu vishkwambi kama motisha, yaani ni mali yao tukiamini watavitumia ipasavyo kama vitendea kazi muhimu na nyie mkifanya hivyo itakuwa ni vizuri kwa kuwa motisha kwa walimu ni kitu cha muhimu sana na ni agizo la Waziri Mkuu," amesema Dkt. Michael

Ameongeza kuwa ni matarajio ya Serikali kuwa vishkwambi hivyo vitakuwa chachu katika kuboresha mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji ili kuinua ubora wa elimu nchini.


Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdulla Said ameshukuru kwa kupatiwa vishkwambi hivyo na kuahidi kuwapatia walengwa mara moja ili waanze kuvitumia kwa ajili ya kuwasaidia katika kazi ya ufundishaji wanafunzi.

"Nina furaha kubwa kupokea vishkwambi hivi na ninaamini vitaleta mapinduzi makubwa sana katika masuala ya Elimu kule Zanzibar.  Nitahakikisha vinagawiwa kwa walimu kama ilivyoelekezwa ili matarajio ya Serikali yatimie," amesema Khamis Abdulla Said.


Kwa upande wake, Prof. Carolyne Nombo, Naibu Katibu Mkuu (WyEST) amesema katika maoni yanayopokelewa ya maboresho ya mitaala ni kuhusu uboreshaji somo la Tehama hivyo  uwepo wa vishkwambi utakuwa ni msingi wa utekelezaji wa uimarishaji ufundishaji wa somo hilo.

No comments:

Post a Comment