MKUU wa Wilaya mpya wa Bahi Godwin Gondwe ameripoti rasmi wilayani humo akitokea wilaya ya Temeke ikiwa ni siku moja baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuongoza Wilaya hiyo.
Gondwe akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi alipokaribishwa, alijinasibu kuanzia pale ambapo mtangulizi wake Mwanahamis Munkunda anayehamia wilaya ya Temeke alipoishia.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM), katika wilaya hiyo ameahidi kushirikiana kikamilifu na viongozi wenzie kutekeleza kikamilifu na kwa vitendo Ilani ya Chama kama alivyofanya Temeke.
Kuhusu Elimu Gondwe amesema anaamini Rais, Samia amempeleka Bahi kwa makusudi na atalifanyia kazi suala hilo kwa vitendo na kuleta tija, kama walivyoweza katika wilaya ya Temeke ambayo kwa mwaka 2022 iliongoza na kushika nafasi ya kwanza Tanzania nzima.
Awali akiaga wajumbe wa Baraza hilo na watumishi wa wilaya mbalimbali,Mkuu wa Wilaya anayeondoka, Mwanahamis Munkunda amesema akiwa Bahi alijifunza mambo mengi na walifanya mengi ya maendeleo akishirikiana na viongozi wenzie aliowakuta, huku akimhakikishia mkuu wa wilaya mpya kuwa Bahi ni mahali pazuri na atapafurahia.
Wakuu wote wa wilaya waliteuliwa na Rais Samia ikiwa ni uteuzi mpya wa watendaji ambao anaamini wataweza kwenda na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita huku wengine wakiachwa.
No comments:
Post a Comment