Na Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia TAMISEMI Ramadhani Kailima amewataka watumishi wote wanaokaguliwa katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa ushirikiano kwa vyombo vinavyofanya ukaguzi.
Akifunga mafunzo ya matumizi ya mfumo wa ukusanyaji wa mapato LGRCIS/TAUSI katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa wadau kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, Jijini Dodoma Kailima amesema kumezuka tabia ya baadhi ya watumishi kutokutoa ushirikiano kwa wakaguzi pindi wanapokuja kukagua baadhi ya miradi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa jambo hilio ni ukiukwaji wa sheria.
Kailima amewasisitiza kuhakikisha wanafafanua hoja kila inapotokea katika muendelezo wa ukaguzi ili ziweze kupatiwa majibu kwa haraka na kupunguza hoja za wakaguzi na ikishindikana zipelekwe ngazi za juu kwa ajili ya kupatiwa majibu
Ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanazichambua hoja zilizojitokeza kwa kuangalia zilizojitokeza kwa mujibu wa mifumo, hoja ambazo haziwezi kukamilika, zilizojitokeza kwa mujibu wa maelekezo ya viongozi na zilizojitokeza kwa mujibu wa sera ili kuweza kuzijibu kwa mujibu wa makundi hayo.
Amewashauri Makatibu Tawala wa Mikoa kuhakikisha wanafanya vikao vya Mocklaac ili kuzichambua hoja zinazojitokeza kwa wakati na kupunguza hoja zinazojitokeza mara kwa mara.
Amevitaka vyombo vyote vya ukaguzi kuhakikisha wanashirikiana na Sekretarieti za Mikoa ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wakitekeleza majukumu yao.
Naye Afisa kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao Mwanaisha Semboko amesema mafunzo hayo yamekuwa na tija kwa taasisi zote za umma zinazoshirikiana kazi na Ofisi ya Rais –TAMISEMI hasa katika suala zima la ukaguzi kwenye mifumo inayotumika kwenye ukusanyaji wa mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuwa imejenga uelewa wa pamoja na kurahisisha utendaji kazi wa wakaguzi.
No comments:
Post a Comment