OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu anayeshughukia Elimu Ofisi ya Rais - TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amesema kuna ongezeko kubwa la wanafunzi wa Elimu msingi na sekondari kufuatia utekelezaji wa Sera ya Elimu bila Ada
Akisoma hotuba kwa niaba yake Mkurugenzi wa Usimamizi wa Elimu Vicent Kayombo amesema Idadi ya wanafunzi wa elimumsingi wameongezeka kwa asilimia 31.4 kutoka 11,877,565 mwaka 2016 hadi 15,609,931 mwaka 2022.
Kayombo ameyasema hayo wakati wa kufungua mafunzo rejea ya Usimamizi wa Mafunzo endelevu ya Walimu Kazini kwa Viongozi na Waratibu wa MEWAKA ngazi za Mikoa na Halmashauri.
Amesema Idadi ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita imeongezeka kwa asilimia 35.9 kutoka 131,362 mwaka 2016 hadi 178,473 mwaka 2022.
Halkadhalika ametanabaisha kuwa Ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.
“Kwa mfano, Ufaulu wa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2016 ulikuwa 70.40% ukilinganisha na mwaka 2021 ambapo ufaulu ulifikia 81.97%. Hata hivyo, matokeo ya mwaka 2022 yameonesha kushuka kwa 2% kwa kupata ufaulu wa 79.6%
Ufaulu wa Mtihani wa Kidato cha Nne umeongezeka kutoka asilimia 70.35 mwaka 2016 hadi asilimia 87.30 mwaka 2021. Hata hivyo, idadi ya wanafunzi wanaopata ufaulu bora wa daraja la I hadi III imefikia asilimia 35 tu (mwaka 2021) alisisitiza Kayombo.
Wakati huo huo Kayombo amesema Serikali inaendelea kuboresha utoaji wa Elimu na sasa kupitia Mradi wa BOOST Shilingi trilioni 1.15 zitatumika kutekeleza afua mbalimbali katika shule za msingi kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa 12,000 na Utekelezaji wa mpango wa shule salama kwenye shule 3,000.
Halikadhalika mradi huu utawezesha uandikishwaji wa wanafunzi wa Elimu ya Awali kutoka asilimia 76.9 hadi 85 na Ununuzi, usambazaji na matumizi ya vifaa vilivyoboreshwa vya kufundishia na kujifunzi Elimu ya Awali kwenye madarasa 12,000
Pia kupitia mradi huu kutafanyika ununuzi , usambazaji na matumizi ya vifaa vya TEHAMA kufundishia na kujifunzia kwenye Shule za Msingi na Vituo vya Walimu 800 amesema Kayombo.
Aidha ameongeza kuwa tutatekeleza mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) kwenye Shule zote 17,182 na Vituo vya Walimu na Utekelezaji wa vigezo vya utawala bora katika Elimu kwenye Halmashauri zote 184 nchini.
Serikali imeshapokea Shilingi bilioni 265.08 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi huu wa BOOST kwa mwaka 2022/23 na kati ya fedha hizo, zaidi ya Shilingi Bilioni 230 zitatumwa moja kwa moja shuleni, kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, na Sekretarieti za Mikoa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi huu.
No comments:
Post a Comment