Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Zaina Foundation, Zainab Njovu akitoa mafunzo juu ya usalamawa mitandao katika semina ya wanahabari wanawake iliyofanyika mkoani Morogoro. Picha na Shua Ndereka |
Na Shua Ndereka Morogoro
Waandishi wa habari wanawake nchini wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa usalama, kufikisha habari zao na kuepuka matatizo mbalimbali yatokanayo na mitandao hiyo pindi inapotumika vibaya.
Hayo yalibainishwa katika semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari wanawake juu ya usalama wa matumizi ya mitandao kidigitali, yaliyofanyika mkoani Morogoro na kuandaliwa na taasisi ya Zaina Foundation kutoka jijini Dar es Salaam.
Akifungua Mafunzo hayo Afisa Mawasiliano na Utawala kutoka Kituo cha Msaada wa Kisheria Mkoani Morogoro Peter Kimath aliwataka wanahabari kuzingatia mafunzo waliyoyapata ili yawasaidie katika kazi zao za kila siku na kuepusha changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwa wanahabari katika usalama wa kimtandao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Zaina Foundation Zainabu Njovu alibainisha kuwa, mafunzo hayo walilenga wanahabari wanawake kwa sababu kazi yao ni muhimu kutokana na vifaa vingi vya wanahabari huhitaji mtandao huku lengo la taasisi hiyo ni kuwawezesha wanawake kutumia teknolojia katika kazi zao za kila siku na kutetea haki ya kidigitali nchini Tanzania.
“Tulilenga kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya mtandao kwa wanawake kutokana na kazi yao inahitaji sana masuala ya mtandao internet na mambo mengine hivyo ni kundi linalohitaji uelewa zaidi juu masuala haya na tunaamini kupitia vyombo vyao vya habari watawaelimisha wanawake wengine sehemu tofauti tofauti nchini.
Kuhusu suala la Mahusiano na ndoa nyingi kuyumba kutokana na matumizi ya Simu, Zainabu aliwashauri wanandoa kuwa waaminifu kwa wenza wao na kuwa na hofu ya Mungu ili kuondoa migogoro mingi inayosababishwa na kifaa hicho kwani inaweza kuwa chanzo cha kupoteza uhai kwa mmoja wao endapo magomvi yakitokea.
Vumilia Kondo ni mmoja wa wanahabari waliopata mafunzo hayo kutoka Mkoani Morogoro anasema kupitia mafunzo haya amejifunza faida kubwa ya kujilinda unapotumia mitandao kwani dunia ipo kiganjani hivyo amewasisitiza wanahabari kutumia mitandao ya kijamii kufikisha habari zao.
Pia ameishukuru Taasisi ya Zainab Foundation kwa kutoa mafunzo hayo katika kundi hilo la wanahabari wanawake kwani itawasaidia kuwa salama pindi wanapotumia mitandao huku akiwaasa wanawake kuendelea kuitafuta elimu zaidi kwa manufaa kupitia mitandao hiyo.
No comments:
Post a Comment