![]() |
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (kulia) akisikiliza taarifa ya usambazaji wa mbolea katika Mkoa wa rukwa kutoka kwa Afisa Masoko wa kampuni la OCP mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Zawadi Hankungwe |
Na Mwandishi wetu Rukwa
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amefanya ziara mkoani Rukwa na kutatua changamoto za wakulima kufuata mbolea maeneo ya mjini pamoja na uwepo wa watendaji wachache kwenye vituo vya mauzo ili kuwawezesha wakulima kuhudumiwa kwa wakati.
Katika ziara hiyo ya siku mbili, Waziri Bashe alitembelea maghala ya mbolea ya kampuni za ETG na OCP na shamba la mbegu la mwekezaji mkubwa la Msipazi Farm lililopo katika Halmashauri ya wilaya ya Nkasi mkoani humo.
Baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Queen Sendiga kueleza nia ya kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa usafiri na kuwahakikishia ulinzi wafanyabiashara ili waweze kupakia na kupeleka mbolea maeneo ya pembezoni na wafanyabiashara kutokukubaliana na wazo hilo, Waziri Bashe aliagiza jambo hilo lifanyike na utekelezaji wake umeanza mapema baada ya maelekezo yake.
Kwa upande wa changamoto ya kupata mbolea ya ruzuku kwa wazalishaji wa mbegu katika scheme ya Msipazi Farm Waziri Bashe alimtaka mwekezaji Yusuph Sumrry kuandika barua ya mahitaji yake ya mbolea kwa Mkurugenzi wa TFRA ili kuyaridhia na kumwezesha kupata mbolea ya ruzuku.
"Andika barua kwa mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhusiana na ombi la kupata mbolea ya ruzuku atakuidhinishia ili wasambazaji wakuletee kiasi cha mbolea mnachokihitaji" Alisisitiza waziri Bashe.
Akikazia katika jambo hilo Waziri bashe alisema nchini kuna changamoto ya mbegu hivyo mwekezaji huyo atasaidia katika kuhakikisha wakulima wanapata mbegu kwa bei himilivu na kwa wakati kuliko kutegemea kuagiza kutoka nje ya nchi.
**Kama una taarifa yako na unatamani tuichapishe kwenye OKULY BLOG basi usisite kututumia kupitia OkulyJulius@gmail.com au +255785364965 kwa WhatsApp au Telegram Karibu sana**
No comments:
Post a Comment