KAIRUKI ATAKA UZINGATIAJI FEDHA ZA MIRADI YA SEQUIP - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 24, 2023

KAIRUKI ATAKA UZINGATIAJI FEDHA ZA MIRADI YA SEQUIP



Na Angela Msimbira, DAR-ES-SALAAM

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki amesisitiza uzingatiaji sahihi wa fedha Sh milioni 600 zinazoelekezwa kwenye miradi ya Mpango wa Kuboresha Elimu ya Sekondari(SEQUIP).

Kairuki ameyasema hayo wakati wa kukagua eneo la ujenzi wa shule ya Kitunda Relini mkoani Dar es Salaam.

Amesema kumekuwapo na sintofahamu ya matumizi ya fedha hizo huku wengine wakitumia fedha hizo nje ya mwongozo katika kujenga shule hizo.

“ Kumekuwa na changamoto kubwa kwenye maeneo mengi ambapo wakiambiwa wamepatiwa kiasi cha shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa shule wanajua kuwa ni ujenzi wa miundombinu ya awali tu hivyo wanajikuta wanazitumia hovyo na baadaye hazimalizi ujenzi na wanadai kuongezewa fedha nyingine, suala hili haliwezekani kwa kuwa tunaamini zinatosha kukamilisha ujenzi huo.”
Amesema Waziri Kairuki


Kairuki amesema kati ya Sh milioni 600 zinazotolewa, Sh milioni 470 zinapaswa kutumika katika ujenzi wa shule kwa kujenga madarasa 8 ya awali, jengo la TEHAMA, jengo la utawala, maktaba, maabara ya fizikia, kemia na biolojia na matundu ya vyoo vya kawaida.

Amesema baada ya kukamilika kwa miundombinu hiyo, Sh milioni 130 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu na Sh milioni 30 kwa ajili ya vifaa vya TEHAMA.

Aidha, Kairuki amewaagiza wahandisi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanasimamia maelekezo hayo ipasavyo na kuwataka wakadiriaji majengo kufanya ukadiliaji ipasavyo.

“Kuna maeneo mengine viwanda vipo karibu vya saruji, nondo hivyo sitarajii kusikia kuwa shilingi milioni 470 hazitoshi rai yangu ni kuhakikisha wanazisimamia ipasavyo ili ujenzi ukamilike kwa gharama hiyo, tunajua fedha hizo zitatosha kwa mujibu wa wataalam,”amesisita Waziri Kairuki

Pia amewaagiza viongozi wote kuanzia ngazi ya Mkoa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ujenzi wa shule hizo ili kutimiza lengo la serikali la kuboresha elimu, kuwapunguzia watoto kutembea umbali mrefu, kuondoa vikwazo kwa watoto kupata elimu na kuhakikisha watoto wa kitanzania wanamaliza masomo yao ya elimu ya sekondari.

Mradi wa SEQUIP umewezesha ujenzi wa takribani shule 232 nchi nzima kwa mwaka 2022 ambapo maeneo mengi ujenzi umekamilika kwa gharama ya Sh milioni 470.

No comments:

Post a Comment