Na Angela Msimbira , DAR-ES-SALAAM
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki ametimiza ahadi yake aliyoitoa Februari 2, 2023 kwenye Mkutano wa Kumi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kutembelea Jimbo la Ukonga, Jijini Dar-es-salaam
Waziri Kairuki amefanya ziara hiyo Februari 23, 2023 ikiwa ni siku 22 tangu alipotamka bungeni kuwa ataambatana na Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mhe. Jerry Silaha kwenda kujionea changamoto mbalimbali wanazokabiliana wananchi ikiwemo changamoto ya barabara ya Banana- Kivule-Msongola.
Waziri Kairuki alianza kwa kutembelea eneo litakapojengwa shule ya Kitunda Relini, kata ya Kitunda Relini ambapo ametoa maelekezo kwa Halmashauri ya Jiji la Dar-es-salaam kulipa fidia kwenye eneo la ekari 2.7 lililochaguliwa kwa ajili ya kujengwa shule hiyo ili ujenzi uanze mara moja
“Niwapongeze kwa kukubali kulipa fidia takribani kiasi cha shilingi milioni 387 kwa ajili ya eneo la kujenga shule ya sekondari Kitunda Relini,hivyo fedha hizo zilipwe kwa wakati kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu,vilevile mzingatie miongozo ya mdhamini Mkuu wa Serikali na kulipa kwa wakati kwa kile kilichoelekezwa kwa mujibu wa taarifa ya mdhamini huyo”amesisitiza Waziri Kairuki
Vilevile, Waziri Kairuki ameendelea kufafanua kuwa kiasi cha shilingi bilioni 1.2 zimetengwa kwa ajili ya miradi wa mpango wa kuboresha elimu ya Sekondari( Secondary Education Quality and improvement programme- SEQUIP) ambazo zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa shule 2 za Sekondari za Kitunda Relini pamoja na Shule ya Sekondari Msongole.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mhe. Jerry Silaa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa katika sekta ya afya,elimu pamoja na miundombinu ya barabara.
Aidha Waziri Kairuki ametembelea Jimbo la Ukonga na kukagua miradi inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar-es-salaam kupitia mapato yake ya ndani pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
No comments:
Post a Comment