Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mh. David Silinde, amesema ofisi hiyo imeanza kupima utendaji kazi wa wakuu wote wa idara na haitosita kuchukua hatua kwa yeyote mwenye utendaji usio ridhisha.
Mh. Silinde amebainishwa hayo leo Februari 23,2023 Mtumba Jijini Dodoma wakati akifungua Kikao kazi cha Makatibu Tawala wasaidizi - Utawala wa Mikoa na wakuu wa Idara ya Utumishi na usimamizi wa Rasilimali watu wa mamlaka za Serikali za Mitaa, kilichokuwa na kauli mbiu isemayo “USIMAMIZI IMARA WA RASILIMALI NI KICHOCHEO CHA UTOAJI WA HUDUMA BORA”.
Amesema kila halmashauri ihakikishe inaandaa mpango wa kutathimini utendaji kazi, mpango wa mafunzo, utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu na mpango wa Rasilimali watu na kuongeza kuwa hayo ndiyo mambo wanayohitaji kila halmashauri kupanga.
Pia Silinde amezungumzia suala la utunzaji wa Siri za serikali ambapo amesema siri hizo zikitoka nje husababisha kudharaulika na pia inaweza kusababisha mgogoro baina ya wananchi na serikali.
“Watu wanatembea na nyaraka hadharani bila kufunikwa, wengine wanaenda nazo nyumbani pia na kuzitoa wanapokuwa kwenye kumbi za starehe na hivyo kusababisha heshima ya usalama wa nyaraka za serikali kutokuzingatiwa na kuhatarisha ustawi wa taifa letu,”amesema Silinde.
Pia ameongeza kuwa serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi wakati wa kushughulikia nidhamu za watumishi hususani yale ambayo wakati wa kushughulikiwa hayakufuata taratibu za uendeshaji.
Awali wakati akimkaribisha Mgeni rasmi ,Naibu katibu mkuu OR -TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amesema kikao hicho kitakachofanyika kwa siku tatu kuanzia leo Feb 23-25 kikafanye kasi ya kuwakumbusha na kuelekezana umuhimu wa malengo waliyo yaweka kama nchi ili kuwahudumia wananchi katika maeneo mbalimbali ya Utumishi wao.




No comments:
Post a Comment