Na Okuly Julius-Dodoma
KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Makampuni na Majina ya Biashara kutoka BRELA Ndg.Meinrad Rweyemamu, ametoa wito kwa wamiliki wa makampuni ,wanasheria na taasisi za kifedha kushiriki katika mafunzo mbalimbali yanayoandaliwa na serikali kuhusu uendeshaji wa makampuni na majina ya biashara yenye ubia.
Ameyasema hayo leo Machi 3,2023 Jijini Dodoma ,wakati akifungua kikao cha kujalidili kuhusu dhana nzima ya wamiliki manufaa katika makampuni na Ubia, baina ya wakala na Wanasheria,Mawakili wa Kujitegemea,Washauri wa biashara na Maafisa wa benki ,kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA ,Godfrey Nyaisa.
Rweyemamu amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa elimu ya namna ya kuwasilisha taarifa za wamiliki manufaa katika makapuni.
"Lengo ni kutaka kusikia changamoto wanazokutana nazo wakati wa kutuma hizo taarifa za wamiliki manufaa kuja BRELA na sisi kama BRELA tutawaambia nini tunazokutana nayo wakati wa kuchakati hizo taarifa na namna ya kutatua hizo changamoto ili twende mbele kwa pamoja,"amesema Rweyemamu
Aidha,Rweyemamu ameongeza kuwa baada ya kikao hicho BRELA inaamini kuwa makampuni mengi yataanza kuwatumia wanasheria kwa ajili ya kuwasilisha taarifa zilizosahihi kuhusu wamiliki manufaa.
"Taarifa za wamiliki manufaa zitakuwa zinatolewa kwa usahihi kwani tunaamini makampuni mengi yatahamasika kutumia wanasheria kuandaa na kutuma taarifa hizo ili kuondoa makosa na taarifa hizi zinatakiwa kuwa siri na hazitakiwi kutapanywa,"amesema Rweyemamu
Kwa upande wake Afisa Programmu kutoka Tanganyika Law Society (TLS) Ofisi ya Dodoma, Mercy Kessy amesema kuwa wao kama Wanasheria,warsha hiyo ni muhimu kwani ukizingatia kwamba usajili wa makapuni unapitia katika sheria mbalimbali hivyo watatumia warsha hiyo kutoa ujuzi wao kwa watu wengine ili nao wapate kujua.
"Sisi kama wanasheria tuna nafasi kubwa sana kwani uanzishwaji wa makampuni unategemea sana sheria mbalimbali hivyo sisi kama wanasheri tutatumia nafasi hii kutoa ujuzi wetu ili wengine nao wapate kujua baadhi ya sheria za umiliki,uanzishwaji wa makampuni,"amesema Kessy
Naye mmoja wa washiriki katika Warsha hiyo Martin Mwailambo kutoka NMB amesema kuwa BRELA imefanya vizuri kuja na semina hiyo kwani itawasaidia kujua habari zaidi kuhusu wamiliki wa makampuni ,kujua biashara zao na taarifa zao kwa ujumla.
"Hili jambo linalofanywa na BRELA ltaleta manufaa sio tu kwa taifa ila hata makampuni pia kwani kwa sasa sheria inataka wale wamiliki wa makampuni wajulikane na biashara zao zijulikane ikiwepo kutuma taarifa sahihi za wamiliki manufaa BRELA kwa ajili ya kuchakatwa,"amesema Mwailambo






No comments:
Post a Comment