DKT.GWAJIMA:VIKWAZO VYA KUTUMIA MITANDAO YA KIDIGITALI VINAWAATHIRI WANAWAKE KWENYE FURSA ZA MAENDELEO. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 6, 2023

DKT.GWAJIMA:VIKWAZO VYA KUTUMIA MITANDAO YA KIDIGITALI VINAWAATHIRI WANAWAKE KWENYE FURSA ZA MAENDELEO.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima,leo Machi 6,2023,Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, ikiwa ni maandalizi kuelekea tarehe 8 Machi 2023 katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima (katikati),leo Machi 6,2023,Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, ikiwa ni maandalizi kuelekea tarehe 8 Machi 2023 katika katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani,(kulia) ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.John Jingu.


Na Okuly Julius-Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa kutokana na vikwazo wanavyokabiliana navyo wanawake kwenye kutumia mtandao wa kidijitali vimewaathiri kwenye fursa za maendeleo na kupata huduma.

Ambapo baadhi ya vikwazo hivy ni pamoja na kushindwa kumudu gharama, kutojua kusoma na kuandika, ukosefu wa ujuzi, ukosefu wa faragha na usalama, maudhui kutokidhi, kutoona umuhimu, kutomiliki, kutofahamu, changamoto za upatikanaji wa nishati ya umeme, mila na desturi na vikwazo vingine.

Dkt.Gwajima ameyasema hayo leo Machi 6,2023,Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, ikiwa ni maandalizi kuelekea tarehe 8 Machi 2023 katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani.

"Tuna kila sababu kama taifa ,kama wizara inayohusika na masuala ya wanawake ya kuhakikisha wanawake wanawezeshwa kidigitali ili kufikia usawa wa kijinsia kwenye maendeleo kwani watumiaji wa huduma za mtandao ambao ni wanaume wana faida kubwa mfano kupata taarifa za afya, elimu, kilimo, biashara, ajira na zingine nyingi,"


Na kuongeza kuwa "idadi ya nchi zinazotoa walau huduma moja ya kijamii kwa njia ya mtandao zimeongezeka kutoka 162 mwaka 2020 hadi 189 mwaka 2022,"amesema Dkt.Gwajima

Waziri huyo amebainisha kuwa takwimu za Dunia kwenye ripoti ya UN-Secretary General kuhusu Kamisheni ya Hali ya Wanawake-CSW 67; inaonekana kuwa, wanawake na wasichana hawanufaiki ipasavyo na teknolojia ya kidigitali mathalani, katika nchi zenye uchumi wa chini 76% ya watu wake wanazo simu zinazopokea mtandao lakini 25% tu ndiyo wanatumia huo mtandao huku 52% wakiwa ni wanaume hivyo wanawake ni wachache zaidi.

Aidha,Dkt.Gwajima amesema pengo la wanawake kumiliki simu na kutumia mtandao linaonekana zaidi kwa wanawake wenye umri mkubwa (wazee), wanawake wanaoishi vijijini pamoja na wanawake wenye ulemavu.


"Mwaka 2022 takwimu zinaonesha 63% ya wanawake duniani walitumia mtandao ukilinganisha na 69% ya wanaume huku uwezo wa wanawake kumiliki simu ukiwa chini kwa 12% ukilinganisha na wanaume,"amebainisha Dkt.Gwajima

Dkt.Gwajima amesema hadi kufikia Februari, 2023 Mikoa 17 tayari imeanzisha Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ,ambapo umessababisha Utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali kuongezeka kutoka Tsh. Bilioni 3.39 kwa vikundi 2,225 mwaka 2015/16 hadi Tsh. Bilioni 111.03 kwa vikundi 34,502 vyenye jumla ya wanawake 996,087 mwaka 2021/22;

"Jumla ya wanawake wajasiriamali 21,546 kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara wamepata mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya Shilingi 78,687,847,568.87 kati ya mwaka 2018/19 hadi 30 Aprili, 2022 kupitia Benki ya TPB (kwa sasa Benki ya Biashara Tanzania Tanzania Commercial Bank),"

Na kumalizia kuwa "Mikopo yenye jumla ya Tsh. 663,436,800/= imetolewa kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali 11 na mwanamke mjasiriamali mmoja mmoja jumla wajasiriamali 14 kuanzia Julai, 2022 hadi Januari, 2023,"amesema Dkt.Gwajima


Ikumbukwe kuwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani kwa Tanzania itaadhimishwa katika ngazi ya mkoa ambapo kila Mkuu wa Mkoa ana wajibu wa kuhakikisha siku hiyo inaadhimishwa na Kaulimbiu ya Maadhimisho ya mwaka 2023 inasema Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia: Chachu Katika Kuleta Usawa wa Kijinsia.

No comments:

Post a Comment