Na. Asila Twaha, Mtwara 
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeridhishwa na usimamizi wa fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili  ukarabati wa shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara.
Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa Mhe. Ester Bulaya (Mb) wakati wa  ziara ya kamati ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika  Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara, Mkoani Mtwara  Machi 29, 2023.
Amesema usimamizi ulioneshwa na uongozi wa shule hiyo ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wote waliopewa  dhamana ya usimamizi wa fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi  ya maendeleo na kuwataka kuwa wazalendo, waadilifu na waaminifu kwa mamlaka walioaminiwa.
Ameutaka uongozi wa shule hiyo kuongeza jitihada katika kuhakikisha wanasimamia na kuitunza shule hiyo na kukuza zaidi taaluma kwa kuwa  Serikali imeshapeleka fedha  kwa ajili ya kuboresha shule hiyo.
Mhe. Bulaya ametoa wito kwa wanafunzi kuonesha jitihada katika masomo  kwa kusoma kwa bidii na kuheshimu walimu  ili waendelee kuwa na ari na moyo katika kutekeleza majukumu yao ili kupatikane viongozi wenye uwezo,elimu,weledi waaminifu na waadilifu.
“Someni kwa bidii najua humu kuna watu wa fani mbalimbali mkiamua mnaweza, ifanyeni shule hii iwe bora  na ninyi ndio mtaifanya ionekane bora kwa kusoma kwa bidii na ufaulu wenu  na kuifanya iweze kuwa bora kama shule nyingine” amesisitiza
Awali akisoma taarifa ya ukarabati wa shule hiyo Mkuu wa Shule Mwl. Sikujua Mangisye amesema, shule ilipokea shs. mil. 776,605,047 na kutekelezwa kwa ukarabati wa majengo 38 ikiwemo  kubadilisha sakafu kwa baadhi ya mejengo, kupiga lipu,  kupaka rangi, kutanua milango na madirisha kwa baadhi ya majengo, kuweka paa jipya kwa baadhi ya majengo, mifumo ya maji taka na safi  na kuongeza mashimo ya maji taka na  mfumo wa umeme kwenye majengo 38.
Ameushukuru uongozi wa shule ya Sekondari Mtwara Ufundi kwa kuwapatia fedha shs.mil. 80,000,000 ambapo waliweza kuunganisha na kiasi cha silingi milioni 82 kilichobaki kwao na kufanya jumla ya shs. mil. 162,000,000 kuanza ujenzi wa mradi wa mabweni mawili ambapo yatawasaidia wanafunzi.
Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Charles Mahera ameupongeza uongozi wa shule kwa usimamizi wa fedha na kuhakikisha ukarabati unatekelezwa kama  maagizo na muongozo wa Wizara ulivyotaka na kuwataka kuendelea  kusimamia na kufanya  suala la elimu linakuwa bora katika mazingira yote ya kujifunzia na kufundishia.
 




 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment