TEKNOLOJIA NA UBUNIFU VYASISITIZWA KUBORESHA SEKTA YA MAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, March 18, 2026

TEKNOLOJIA NA UBUNIFU VYASISITIZWA KUBORESHA SEKTA YA MAJI




Na Shua Ndereka, OKULY BLOG- Morogoro


Serikali imesema itaendelea kuongeza uwekezaji katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya maji nchini, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha na endelevu kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Maji yanayofanyika mkoani Morogoro, ambapo amesema, uwekezaji thabiti katika miundombinu ya maji ni hatua muhimu ya kukabiliana na changamoto za uhaba wa maji zinazoweza kujitokeza katika vipindi mbalimbali.

“Kama serikali tutaendelea kuwekeza katika miundombinu ya maji, na kuwa na uendelevu wa maji ili kutotegemea maeneo machache, ili nchi yetu iwe na utunzaji mkubwa wa maji na kuendelea kujiandaa na akiba ya maji”.

Kairuki amewahimiza wadau wa sekta hiyo, kuendeleza ubunifu kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuboresha huduma za maji.

Aidha katika maadhimisho hayo ya Wiki ya maji yamekuwa na Mdahalo wa kitaifa wa wadau kuhusu Maji na Jinsia ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema mdahalo huo ni jukwaa muhimu linalowawezesha wadau kujadiliana na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha sera na mipango ya sekta ya maji nchini.

Amesisitiza kuwa, ushirikiano wa wadau mbalimbali ni nguzo muhimu katika kuhakikisha huduma za maji zinapatikana kwa usawa na kwa njia endelevu kwa wananchi wote.

Naye Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga, amesema kamati hiyo itaendelea kusisitiza umuhimu wa kuzingatia usawa wa kijinsia katika upangaji wa sera, mipango na utekelezaji wa miradi ya maji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Sera, Utetezi na Ushawishi kutoka Taasisi ya WaterAid Tanzania Christina Mhando amesema kuwa, upatikanaji wa maji safi na salama ni msingi muhimu wa kufikia usawa wa kijinsia, kuboresha ustawi wa jamii na kuchochea maendeleo endelevu nchini.

“Suala la kijinsia ni moja ya mageuzi makuu kwa WaterAid, ili kufikia maji kwa wote kila mahali, ambapo tumekuwa tukiweka kipaumbele suala la jinsia kwa kila miradi tunayotekeleza ikiwemo suala la maji, kwa kutambua kwamba uwekezaji katika huduma za maji, si suluhisho la kiufundi bali ni kichocheo cha haki, heshima, usawa wa fursa na mabadiliko ya kijamii”. Amesema

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amepongeza juhudi za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya maji, akibainisha kuwa hatua hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma ya maji kwa uhakika kwa wananchi.

Maadhimisho ya wiki ya Maji kila mwaka nchini, huanza Machi 16 na kufikia kilele chake Machi 22, 2026 siku ambayo Dunia huadhimisha siku ya Maji, ambapo yamebebwa na Kaulimbiu isemayo ‘Maji na Jinsia’ ikilenga kuhamasisha usawa wa kijinsia katika usimamizi, upatikanaji na matumizi ya rasilimali za maji.

Hata hivyo maadhimisho ya siku ya Maji kitaifa kwa mwaka huu 2026, yatafanyika katika mkoa wa Morogoro, ikiwa ni kitovu cha kuzalisha maji na vyanzo vingi ikiwemo mito inayolisha mto Ruvu ambao ni tegemeo na manufaa ya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment