Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. John Jingu kufuatilia utekelezaji wa mchakato wa Sheria ya Maafisa Ustawi wa Jamii itakayoainisha miiko na maadili ya utoaji wa Huduma za Ustawi wa jamii nchini.
Waziri Dkt. Gwajima ametoa agizo hilo wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo chenye lengo la kupitia utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Mpango wa bajeti ya Mwaka 2023/24 kilichofanyika jijini Dodoma Aprili 12, 2023.
Amesema sheria hiyo itaimarisha utendaji kazi wa Maafisa Ustawi wa Jamii hata wa sekta binafsi kufanya kazi za ustawi katika misingi ya maadili kwani watatambulika na kuisaidia jamii kwa upana wake.
Mhe.Dkt. Gwajima pia amesisitiza watumishi kujihadhari na mmomonyoko wa maadili unaopelekea ukatili wa kijinsia na kwa watoto na kuwa mstari wa mbele kukemea maovu katika jamii.
"Ni gharama kubwa kupoteza mfanyakazi kutokana na kukutwa na makosa ya kisheria ambayo yanaepukika. Tuwe waadilifu kwa mila na tamaduni zetu, tuwaibue wanaoenda kinyume na kuchochea mmomonyoko wa maadili unaoharibu mila na tamaduni zetu na hatimaye kuibuika kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kwa watoto" amesema Waziri Gwajima.
Aidha, Mhe.Dkt. Gwajima ameelekeza kuundwa na kuyatumia madawati ya jinsia kwenye maeneo ya kazi hasa kwa Taasisi zilizo chini ya Wizara ifikapo 30 Aprili 2023 ili kuwa na sehemu sahihi kwa watumishi kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwani na wao pia wanakumbana na vitendo hivyo katika maeneo ya kazi.
Ameongeza kwamba watumishi wa Wizara hiyo wanatakiwa kutumia elimu na ujuzi walionao kubuni namna bora ya kukabiliana na changamoto zilizopo na kuendelea kubadilisha changamoto kuwa fursa.
Halikadhalika ameeleza kwamba, ni wakati muafaka kwa Wizara kuutumia kikamilifu Mkataba wa huduma kwa mteja ili kutoa huduma bora kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo kwenye mkataba huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Katibu Mkuu Dkt. John Jingu amesema kikao hicho kitajadili na kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Mwaka wa fedha uliopita, ikiwemo kuangalia changamoto zilizojitokeza na kuchukua hatua.
"Mhe. Waziri baada ya kikao hiki tegemea mabadiliko makubwa katika utendaji wa Wizara yetu, tutahakikisha tunajadili kama Timu Moja kwa lengo kuleta ufanisi na tija" amesema Dkt. Jingu.
Naye mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo Dora Neema George amesema matarajio yao kama wafanyakazi wa Wizara ni kuona bajeti yenye kutosheleza mahitaji ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vilivyopo kwenye bajeti.
No comments:
Post a Comment