
Na Okuly Julius , DODOMA
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimefungua rasmi kambi maalum ya elimu, uchunguzi wa afya, na utoaji wa huduma za matibabu bure kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Kongamano la Afya litakalofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 13 Juni 2025.
Kambi hiyo inafanyika katika Kituo cha Afya Hombolo kwa muda wa siku mbili—leo na kesho—na inalenga kuwahudumia zaidi ya watu 1,500. Huduma zinazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa afya, ushauri wa kitabibu, na matibabu ya awali kwa wananchi wote wanaofika kupatiwa huduma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaaluma, Prof. Razack Lokina, alisema kuwa kambi hiyo ni sehemu ya mchango wa chuo katika kutatua changamoto za kiafya kwa kutumia ushahidi wa kitaalamu na tafiti—ambavyo ndio msingi mkuu wa kongamano hilo.
“Kwa kushirikiana na wataalamu bingwa kutoka Hospitali ya UDOM na Chuo Kikuu cha Dodoma, tunatoa huduma hizi kwa jamii ili kuwasaidia wananchi kupata huduma bora za afya, huku tukitumia fursa hii kukuza uelewa wa masuala ya afya na elimu,” alisema Prof. Lokina.
Prof. Lokina aliongeza kuwa maandalizi ya kongamano hilo, linalotarajiwa kukutanisha zaidi ya washiriki 500 kutoka ndani na nje ya nchi, yalianza rasmi Jumamosi iliyopita kwa kuandaa matembezi ya hiari ya “Fun Run” yaliyoshirikisha wadau mbalimbali kutoka taasisi na mashirika tofauti—ikiwa ni ishara ya mshikamano katika kukuza afya na ustawi wa jamii.
Kwa wananchi watakaobainika kuhitaji matibabu ya juu zaidi, watarejelewa katika hospitali kubwa ndani ya Jiji la Dodoma ili kupatiwa huduma za kibingwa kwa kina.
Kongamano la Afya 2025 linatarajiwa kuangazia mada kuu ya:
“Matumizi ya Ushahidi wa Utafiti na Ubunifu katika Kutatua Changamoto za Afya Nchini”
Kongamano hili litaunganisha wataalamu wa afya, watafiti, wanafunzi, na wadau kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kubadilishana maarifa na uzoefu katika kuboresha sekta ya afya nchini.
Kwa upande wake, Mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Afya ya Jamii wa UDOM, Bw. Leonard Katarambura, alisema kuwa kambi hiyo imepelekwa Hombolo kwa kuwa ni eneo lenye watu wengi linalohitaji huduma za afya, na pia ni sehemu ya jamii inayozunguka chuo.
“Tumeleta huduma hizi hapa Hombolo kwa kuwa ni sehemu ya Jiji la Dodoma yenye watu wengi, na pia kuna wananchi ambao hawana uwezo wa kufika hospitali kubwa kupata huduma za kibingwa. Hapa tunawaletea huduma hizo moja kwa moja kupitia ushirikiano wa madaktari bingwa kutoka UDOM na Hospitali ya Benjamin Mkapa,” alisema Katarambura.




No comments:
Post a Comment