Na WMJJWM,DSM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuna kila sababu ya kutumia mbinu mbadala kuhakikisha taarifa za fursa mbalimbali za maendeleo zinawafikia wananchi.
Ameyasema hayo Aprili 29, 2023 alipokuwa akihitimisha Tamasha la Maendeleo la kutangaza fursa za kiuchumi na kupinga ukatili lenye kaulimbiu ya ZIFIUKUKI (Zijue Fursa Imarisha Uchumi Kataa Ukatili Kazi Iendelee) kwa mkoa wa Dar es salaam.
"Tuna ajenda nyingi sana lakini ajenda ya maadili inapaswa kuwa ajenda ya kipaumbele kwani, iwapo familia haina maadili ni sawa na kutokuwa na familia kabisa. Tuliangalia sababu za mmomonyoko wa maadili tukaona mbali na malezi na makuzi na utandawazi pia ni changamoto ya uchumi" amesema Dkt. Gwajima.
Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali na Wadau imeona katika kupambana na suala hilo ni vema pia kuzungumza na wananchi lugha ya kiuchumi kwa kuwasogeza karibu na fursa za mikopo nafuu, mafunzo, masoko ya bidhaa zao na ajira.
"Mpango wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kila Mwananchi anafikiwa na fursa za kiuchumi" ameongeza Waziri Dkt. Gwajima.
Aidha, Mhe. Gwajima ametoa wito kwa Wadau kujitokeza kushirikiana kuandaa matamasha hasa ngazi ya kata, mtaa na vijijii ili wengi washiriki na kukutana na fursa ambazo sio rahisi kwao kuzifikia.
Halikadhalika, amewashukuru Wadau wote wa Mkoa wa Dar es Salaam walioshirikiana na Wizara kuandaa Tamasha hilo muhimu ambalo litaendelea kufanyika katika mikoa yote nchini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saadi Mtambule amesema wataendelea kuibeba ajenda ya ukatili na kuimarisha uchumi kwa kuimarisha Uratibu, kuwaunganisha Wajasiriamali na Taasisi za fedha pamoja na mifumo ya kidijitali
"Wadau wote mliokuja hapa tunawashukuru kwa moyo na utayari wa kubeba ajenda ya ukatili wa kijinsia. Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazofanya kuweka mazingira mazuri ya kiuchumi kwa Makundi yote.
Changamoto ya ukatili wa kijinsia kwa kiasi kikubwa inachangiwa na wengi kutokuwa na uwezo wa kutengeneza ajira na kipato hali iinayochochea unyonge na ukatili hasa kwa Wanawake" amesema Mtambule.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge ameishukuru Wizara na Wadau kwa kuzindua Tamasha hilo katika Wilaya ya Kinondoni na kwamba kuanza kwa Tamasha hilo kutafungua fursa kwa matamasha mengine Wilaya hiyo na Mkoa.
Nao baadhi ya washiriki waliopata nafasi ya kuonesha fursa zinazopatikana wametoa wito kwa wananchi wote kutafuta taarifa sahihi za kuwasaidia kuinuka kiuchumi ikiwemo kushiriki matamasha kama hayo.
No comments:
Post a Comment