WAZIRI MKUU AIPONGEZA WIZARA YA MAJI KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, April 29, 2023

WAZIRI MKUU AIPONGEZA WIZARA YA MAJI KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI.


Na Okuly Julius -Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameisifu Wizara ya Maji namna ilivyojipanga vizuri katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini kwa lengo la kufikisha maji hadi kwenye vitongoji nchini.


Waziri Mkuu akifungua Semina kwa Wabunga kuhusu Sekta ya Maji Bungeni Dodoma jana alisema, wizara ya maji kwa kujipanga huko moja kwa moja inatekeleza maagizo ya Ilani ya CCM pamoja na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa wakati anafungua Bunge mwaka 2021.


"Wizara imejipanga kupitia mpango kazi wake, kufanya jitihada za kufikisha maji katika vitongoji," alisema.


Wizara kwa kuweka mpango kazi wake imeweza kutekeleza na kukamilisha miradi mipya na imekwamua miradi iliyokwama na kuhakikisha inafanya kazi na kutoa huduma ya maji kwa wananchi.


Kwa kutekeleza miradi hiyo, imesaidia binadamu na viumbe mbalimbali vinavyohitaji maji kupata huduma hiyo katika maeneo yao.


Waziri Mkuu amesema wizara hiyo, imefanya maboresho mbalimbali kwenye halmashauri kwa kubadili mfumo wa utoaji huduma ya maji kwa kuunda Mamlaka ya Maji Vijijini (RUWASA) ambayo ina jukumu la kusimamia na kusambaza maji kwa uhakika katika ngazi za wilaya hadi vijijini.



Kampeni ya kulinda vyanzo vya maji inatakiwa kuwa shirikishi zikiwemo ofisi ya Rais, Makamu wa Rais na wizara, taasisi na idara mbalimbali ili wizara ifanikishe azma yake ya kufikisha maji hadi kwenye vitongoji.


Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema, wizara hiyo imejipanga vizuri kuondoa kadhia za maji nchini na imefanikiwa kutekeleza hilo kutokana na Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha za kutosha katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini.


Aweso amesema wizara hiyo itahakikisha inatekeleza maagizo ya Ilani ya CCM ya kusambaza maji hadi ifikapo mwaka 2025 kwa asilimia 85 vijijini na mjini kufikia asilimia 95, akaahidi wizara hiyo kutokuwa kikwazo kufikia malengo hayo.



Awali akitoa taarifa ya utendaji wa Wizara ya Maji, Naibu Katibu Mkuu Cyprian Luhemeja alisema wizara hiyo imejipanga vizuri katika kuangalia vyanzo vya maji, usambazaji pamoja na ubora wa maji.


Tanzania ipo salama haina changamoto ya vyanzo vya maji bali ina changamoto ya usambazaji kwani kuna maji mita za ujazo bilioni 126, kati yake meta za ujazo bilioni 105 zipo juu ya uso wa dunia na mita za ujazo bilioni 21 zipo chini ya ardhi.


Semina hiyo imefungwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ambaye aliwataka wabunge watumie mada walizopatiwa katika semina hiyo kujadili bajeti ya wizara ya maji inayokuja bungeni karibuni.

No comments:

Post a Comment