Mhadiri kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Tekinolojia ya Nelson Mandela Dkt. Cecilia China (Kulia) akionyesha dawa ya asili ya kusindika ngozi ambayo inasaidia kuondoa matumizi na utegemezi wa kemikali kutoka nje kwa wananchi waliotembelea banda la taasisi hiyo wakati wa Maonesho ya Wiki ya Ubunifu katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Afisa Usimamizi wa Tafiti kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Tekinolojia ya Nelson Mandela Bw, Okuli Andrea akieleza jambo kwa mwananchi aliyetembelea banda la taasisi hiyo wakati wa Maonesho ya Wiki ya Ubunifu katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Baadhi ya Bidhaa zilizotengenezwa dawa ya asili ya kusindika ngozi ambayo inasaidia kuondoa matumizi na utegemezi wa kemikali kutoka nje iliyobuniwa na Mhadhiri kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Dkt. Cecilia China.
Na Mwandishi Wetu-DODOMA
Mhadhiri kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Tekinolojia ya Nelson Mandela Dkt. Cecilia China amebuni dawa ya asili ya kusindika ngozi ambayo itasaidia kuondoa matumizi na utegemezi wa kemikali kutoka nje.
Dkt. Cecilia alisema hayo wakati wa Maonesho ya Wiki ya Ubunifu yaliyofanyika Jijini Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri yaliyoanza Aprili 24 hadi aprili 28,2023 ,ambapo alieleza kuwa ubunifu wa dawa hiyo ambayo imetengenezwa kwa kutumia mitishamba itasaidia kutatua tatizo la upatikanaji wa kemikali za kusindika ngozi.
“Kwa sasa hapa nchini hatuna kiwanda cha kuzalisha kemikali za kusindika ngozi tunaingiza hizi dawa kutoka nje na wajasiriamali wengi ambao wanasindika ngozi na ambao ni wengi hawana uwezo wa kumudu zile dawa kwasababu viwanda vyao vidogo.” amesema Dkt. Cecilia.
Alisema pia matumizi ya dawa isiyo na kemikali itasaidia katika utunzaji mazingira.
“Hata ikitokea mtu amepata hizo dawa, hana uwezo wa kusafisha majitaka kwasababu hawana miundombinu mizuri na zile dawa ni sumu na matokeo yake wanaishia kufungiwa.”Dkt.Cecilia.
DkT. Cecilia alisema ubunifu huo aliouanza akiwa anasoma shahada yake ya Uzamivu (PhD) katika Taasisi hiyo, ulipata ushindi wa kwanza katika kundi la vyuo vikuu wakati wa MAKISATU ya mwaka 2020.
“Hiyo ilinipa fursa ya kufadhiliwa na COSTECH kwa ajili ya kuendelea, fedha nilizopewa ziliwezesha kubuni mtambo wa kutengeneza dawa na kuilinda kisheria.” Dkt. Cecilia
Alisema kupitia mradi wa Kongani Bunifu COSTECH ilimfadhili ili kuhamisha teknolojia kwa kikundi cha wasindika ngozi chenye wanachama 15 kilichomo Usangi mkoani Kilimanjaro.
Aidha, Dkt. Cecilia alisema kwa sasa wanampango wa kusajili kampuni ya jamii ambayo itahusika kutengeneza dawa kwa ajili ya wajasiliamali wadogo, kufundisha namna ya kutumia na kutafutiwa masoko.
Alisema pia Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknoloji ya Nelson Mandela tayari imefanya upembuzi yakinifu wa soko la dawa hiyo na kugundua kuwapo kwa mahitaji makubwa.
Anazidi kueleza kuwa ili kuongeza uzalishaji unahitajika mtambo wenye thamani ya Sh. milioni 500 hatua ambayo itasaidia kutosheleza soko la ndani na kuunza nje ya nchi.
“Tunahitaji mtambo mkubwa ambao thamani yake ni takribani shilingi milioni 500 ili tuweze kuzalisha dawa inayoweza kukidhi mahitaji. Na uwekezaji huu unaweza kulipa ndani ya miaka mitatu.” Alisema Dkt. Cecilia.
“Lengo letu ni tuchangie kwenye mnyororo wa thamani wa ngozi hasa kutokana na Tanzania kuwa nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika na tumekuwa tunazalisha ngozi takribani milioni 11 lakini asilimia 80 mpaka 90 tunaziuza nchi za nje zikiwa mbichi.” Alisema Dkt. Cecilia
Alisema pia uongezaji thamani ngozi utawezesha nchi kupunguza uingizaji wa viatu vya plastiki ambapo kwa sasa mahitaji ni mpaka milioni 60 na uzalishaji wa ndani ni jozi milioni 1.2 za viatu.
“Sasa kwanini tusitumia tekinolojia za ndani na malighafi za ndani tukaongeza thamani ya ngozi, tukazalisha viatu na watanzania wakavaa. Sisi tunataka tuchangie kwenye sekta ya ngozi iweze kukua kwasababu inauwezo wa kuajiri vijana wengi.”Alisema Dkt. Cecilia
Naye Afisa Usimamizi wa Tafiti kutoka Taasisi hiyo, Okuli Andrea alisema Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Tekinolojia ya Nelson Mandela imejikita katika kutoa shahada za Uzamili na Uzamivu na kufanya tafiti mbalimbali za kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
“Katika maonesho ya Wiki ya Ubunifu mwaka 2023 tumekuja na bunifu mbalimbali ambazo zinatatua changamoto katika jamii ambazo ni bidhaa za ngozi zisizotumia kemikali, ngwara yenye virutubisho, vyakula lishe na mtambo wa kusafisha maji na bidhaa nyingine mbalimbali.” Alisema Bw. Okuli
No comments:
Post a Comment