VYANZO VYA MAJI MOROGORO, HATARINI KUFUATIA UCHIMBAJI WA MADINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, February 3, 2026

VYANZO VYA MAJI MOROGORO, HATARINI KUFUATIA UCHIMBAJI WA MADINI



Na Shua Ndereka, Morogoro


Shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini zimeendelea kusababisha uharibifu wa vyanzo vya maji katika Mkoa wa Morogoro, hali inayotishia upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

Tatizo hilo limeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wametoa onyo kali kwa wanaohusika na shughuli hizo.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Morogoro, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Mhandisi Joseph Masunga, amesema uchimbaji wa madini unaofanyika karibu na vyanzo vya maji unasababisha uharibifu wa mazingira, kuchafua maji na kupungua kwa vyanzo hivyo vya maji.

Amesema hali hiyo inaathiri moja kwa moja maisha ya wananchi kwa kusababisha uhaba wa maji, kuongezeka kwa gharama za kuyapata, pamoja na kuhatarisha afya kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama.

“Tulichokiona ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kupitia miradi mbalimbali ya maji, sasa haya yanayofanyika katika Bwawa la Mindu kule, ni kinyume na kanuni za uhifadhi wa mazingira kwani shughuli zinazofanyika kule ni uchimbaji wa madini ambazo zinaathiri ubora wa maji kutokana na sumu zinazopatikana wakati wa uchakataji wa madini yanayochibwa” amesema Joseph Masunga.

Pia amewataka wachimbaji kuheshimu sheria za uhifadhi wa mazingira na kusitisha mara moja shughuli zinazohatarisha vyanzo vya maji ili kuhakikisha maji yanakuwa salama na kupatikana kwa wingi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), CPA Sais Kyejo, amesema Serikali imelazimika kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 1.3 katika kata za Kiegeya, Mkundi na Lukobe ili kurejesha na kuimarisha huduma ya maji safi na salama.

Uwekezaji huo umehusisha ujenzi wa kulaza miundombinu ya mabomba ya maji, huku akibainisha kuwa, uharibifu wa vyanzo vya maji unatishia uwekezaji huo na kuisababishia Serikali hasara kubwa.

“Kwa sasa tumefanya uwekezaji mkubwa kwa eneo la Kingolowira, tumekamilisha mradi mkubwa wa usambazaji wa maji hata maeneo mengi yaliyokuwa hayapati huduma tyari tumelaza mabomba, tumekamilisha kazi kule Kologoso ambako hakukuwahi kuwa na miundombinu ya maji”. Amesema CPA Sais Kyejo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmassy, amesema uharibifu wa vyanzo vya maji una madhara ya muda mfupi na mrefu ikiwemo kuongezeka kwa ukame, migogoro ya matumizi ya maji na kuharibika kwa ikolojia ya mazingira.

Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kupanda miti, kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, pamoja na kuwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli mbadala za kiuchumi ili kupunguza utegemezi wa shughuli zinazoharibu mazingira.

Hata hivyo uharibifu wa vyanzo vya maji unaotokana na uchimbaji holela wa madini ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali, wachimbaji na jamii kwa ujumla kwani uhifadhi mazingira ni wajibu wa kila mmoja ili kulinda maisha ya sasa na ya vizazi vijavyo.






No comments:

Post a Comment