Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam Dalmia Mikaya amezindua rasmi mradi wa Elimu ya Mirathi Mashuleni ulio chini ya Taasisi isiyo ya kiserikali ya Mirathi Tanzania (MITA)lengo likiwa kuipeleka elimu hiyo kwa jamii ya Wilaya hiyo na Watanzania kwa ujumla.
Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika leo Februari 3,2026 katika Shule ya Sekondari Nguva Wilayani Kigamboni na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Wilaya hiyo, walimu na wanafunzi wa shule hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Ofisa Tarafa Wilaya ya Kigamboni Agusta Safari aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo amesema programu hiyo inalenga kukuza uelewa wa msingi wa sheria za Mirathi, haki ya kurithi na taratibu za kimahakama pamoja na kupunguza migogoro ya kifamilia ili kulinda haki za wajane na yatima.
"Kauli mbiu ya programu hii inasema "Mirathi ni Amana, Linda Haki ya Mjane na Yatima. Wazo hili limekuja wakati muafaka kwa kujenga jamii yenye kuheshimu msingi imara wa kufikia dira ya maendeleo ya Taifa 2050.
Amefafanua kwa kutoa elimu hiyo mashueni ni dhahiri itafika kila kaya yenye watoto mashuleni na hivyo kupa wigo wa uelewa wa masuala ya mirathi na taratibu za kimahakama.
"Tumeshuhudia mara nyingi familia zikisambaratika baada ya wazazi kufariki, migogoro ya mirathi imekuwa moja ya chanzo cha baadhi ya watoto wetu kuishia njiani kimasomo kwa kukosa ada na mahitaji muhimu," amesema.
Aidha amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya kiongozi wake Rais, Dk.Samia Suluhu Hassan imejikita katika kusimamia haki za wanyonge, hususan wanawake na watoto, huku akiiona kampeni hiyo kama sehemu muafaka ya kufanikisha hilo.
Mradi huo ambao ni wa kwanza nchini umejikita katika kujenga uelewa wa suala zima la mirathi, ulinzi dhidi ya dhuluma za mali, na kuhamasisha utamaduni wa kuandika na kutunza wosia.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Shirika wa Shirika la Mirathi Tanzania(MOTA) Rose Fussi amesema mradi huo ni chachu katika kuelekea dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ili kujenga jamii yenye uelewa wa sheria, na usawa wa kijamii na kiuchumi.
"Imani yetu ni kwamba, kwa kila mtoto mmoja katika kila familia atakaepata elimu hii, atarudi kwenye familia yake kama balozi wa kueneza elimu hii, na ndio maana tumejikita mashuleni,"amesisitiza Fussi ambae pia ni mtaalamu wa sheria.






















No comments:
Post a Comment