KAIRUKI AWASHUKURU UNFPA,SERIKALI YA DENMARK, UBORESHAJI WA KITUO CHA AFYA DABALO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 10, 2023

KAIRUKI AWASHUKURU UNFPA,SERIKALI YA DENMARK, UBORESHAJI WA KITUO CHA AFYA DABALO


OR-TAMISEMI, CHAMWINO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Angella Kairuki ameshukuru Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kupitia mradi wa kuboresha huduma za afya ya uzazi, watoto na vijana (RMNCAH - UNFPA) uliyofadhiliwa Serikali ya Denmark kwa kuwekeza fedha kwa ajili ya maboresho ya Kituo cha Afya Dabalo kilichopo Halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma


Kairuki ametoa shukrani hizo Mei 09, 2023 katika hafla fupi ya makabidhiano ya jengo la upasuaji, wodi ya wazazi, vifaa na vifaa tiba pamoja gari la kubebea wagonjwa katika Kituo cha afya Dabalo Wilayani Chamwino.



Amesema gharama za uwekezaji huo ni jumla ya Sh 615,205,539 ambapo Sh 327,000,000 zimetumika kwa ukarabati na ujenzi na Sh 288,205,539 zimetumika kwa ununuzi wa gari la kubebea wagonjwa na vifaa/vifaa tiba


"Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, natoa shukrani zangu za dhati kwa kuboresha huduma za afya nchini hasa huduma ya mama na mtoto, ni matumaini na matarajio yangu kuwa uwezeshaji huu utaleta mwanga mpya wa matumaini kwa jamii ya Chamwino kwa ujumla" Amebainisha Kairuki



Aidha Waziri Kairuki amezitaka Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuwa na matumizi sahihi ya magari ya kubebea wagonjwa ikiwa ni pamoja na kuliwekea bima na kuyafanyia matengenezo kinga kwa wakati na mara kwa mara.


Pia amezitaka Mamlaka hizo kuhakikisha kuwa vituo vyote vya afya vilivyojengwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo vinatoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.



Ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya zinakidhi vigezo kwa mujibu wa Miongozo iliyotolewa na Serikali ,Kairuki amezitaka Mamlaka hizo kufanya usimamizi saidizi wa ubora wa huduma katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika maeneo yao.


Awali, Mwakilishi wa UNFPA nchini Tanzania, Mark Bryan Schreiner alisema kuwa wanatambua dhamira ya pamoja na Serikali ya Tanzania kutoa haki na chaguo kwa wote, na kwamba wanaheshimu kujitolea kwa wahudumu wa afya katika kutoa huduma za afya ya uzazi na jinsia.



“Tunaitambua Serikali ya Denmark kama mtetezi dhabiti wa kimataifa wa afya ya uzazi na haki za uzazi, na Ubalozi wa Kifalme wa Denmark jijini Dar es Salaam kwa kusaidia uimarishaji wa mfumo wa afya ili kupanua uwezo wa huduma za afya ya uzazi nchini Tanzania.


“Tunaishukuru Serikali ya Denmark kwa ufadhili wa dola za Marekani milioni 2.3, ambazo zilisaidia mradi wa Kutambua Upatikanaji wa Haki za Afya na Haki za Ujinsia na Uzazi Vijijini hapa Tanzania. Shughuli nyingi za mradi zilifanywa kutoka 2019 hadi 2021,”amesema Schreiner.


Balozi wa Denmark nchini, Mette Norgaard amesema: “Kupitia utoaji wa huduma za afya ya uzazi na taarifa, mradi unaofadhiliwa na Denmark umeleta mabadiliko katika maisha ya makumi ya maelfu ya wanawake, wanaume na vijana,” amesema.

No comments:

Post a Comment