Na Okuly Julius-Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema kazi ya kukusanya maoni ya kuboresha mitaala na sera ya elimu inaendelea, watachakata maoni yote yaliyotolewa na wadau ili kupata kitu kizuri chenye tija kwa taifa.
Prof.Mkenda ameyasema hayo Leo Mei 14,2023,Jijini Dodoma wakati wa Kongamano lilioduma Kwa siku tatu tangu Mei 12-14 la kujadili Sera ya Elimu na Mafunzo kuhusu uhuishaji wa sera na Mitaala ya Elimu ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center.
“Suala kubwa kama hili hatuwezi kukurupuka. “Kazi ya kukusanya maoni inaendelea , tumesikiliza maoni mengi, na sisi tutaangalia na kufanyika kazi kwani kwenye sera kikitamkwa lazima tutekeleze,” alisema
“Kwenye sera ya elimu, mapitio ya sera ni sekta yote ya elimu inagusa kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vya ualimu lakini katika mitaala tutagusa elimu ya awali msingi, sekondari, elimu ya ualimu, vyuo vya serikali na binafsi, huku kwenye elimu ya vyuo vikuu TCU ndio watakaoshughulika kupanga mitaala.
“Tuhakikishe tunapowafundisha watu VETA tukienda kwenye gereji tuwakute huko, kazi ya mitaala inaendelea na itakuwa endelevu siku zote, kazi tetu kubwa ni kujenga elimu ya kujitegemea,” alisema
Prof.Mkenda amesisitiza kuwa mafunzo ya amali yasiwe kwa ajili ya waliofeli, kutakuwa na shule za kilimo kwa mitaala mipya, pamoja na shule za michezo za serikali zitakazoanzishwa ili kulitekeleza hili.
Amesema kwa sasa wataanza na shule tisa zilizopo hawatafanya kwa kukurupuka bali hatua kwa hatua ili suala hili kubwa lifanikiwe.
Pia amesema serikali ya mapinduzi ya Zanzibar nayo inadfanya mapitio kwa mambo ambayo sio ya muungano.
Akifunga Kongamano hiyo,Naibu Waziri wa OR-TAMISEMI Mhe.Deogratius Ndejembi amewataka wadau wote wa Elimu kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika safari waliyoianza ya maboresho ya Sera na Mitaala ya Elimu hapa nchini.
Amesema kazi inayofanywa na Wizara hiyo ni Kwa ajili ya maendeleo ya Taifa hivyo OR-TAMISEMI ipo tayari kutekeleza Sera zote zitakazotolewa ili kuchochea maendeleo ya Elimu Kwa ujumla.
"Nitoe Rai Kwa Wadau wote wa Sekta ya Elimu kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa Kwa Wizara ya Elimu katika kipindi Hiki Cha kupitia na kuboresha Sera na Mitaala kwani tukiwa na Sera madhubuti ya Elimu itapelekea hata wahitimu wetu kuwa Bora na kuweza kujiajiri na kuajirika Kwa urahisi Kwa wanakuwa wamepita katika misingi sahihi ya Elimu,"amesema Mhe.Ndejembi
Aidha,Mhe.Ndejembi amebainisha kuwa OR-TAMISEMI Kwa kuonesha umuhimu wa Mabadiliko haya ya Sera na Mitaala inakwenda kujenga Shule za Ufundi katika Halmaushiri zote ambazo hazijafikiwa na VETA.
"Ofisi ya RAIS TAMISEMI ni pacha wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kazi yetu kubwa ni kusimamia na kutekeleza Sera zinazotolewa katika Elimu maana sisi ni wamiliki wa shule zote za Serikali hivyo tuna wajibu mkubwa wa kuhakikisha Elimu inayotolewa ni Bora na Kwa kudhihirisha Hilo tunakwenda kujenga Shule za Ufundi Kila Halmashauri ambayo hakuna VETA na Mafunzo ya Amali yatatolewa pia huko vyeti vitatolewa ambavyo ni SAWA kabisa na vile vinavyotolewa VETA,"ameeleza Mhe.Ndejembi
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof.Carolyne Nombo, amesema michango iliyotolewa na wadau itazingatiwa kwenye uchakataji ili kuwa na sera na mitaala bora.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya Bunge, Elimu, Utamaduni na Michezo, Prof.Kitila Mkumbo, alisema kazi yao ni kuhakikisha wanasimamia serikali kutekeleza mambo yaliyomo kwenye rasimu za sera na mitaala na yaliyoshauriwa na wadau.
Amempongeza Rais Samia kwa utashi na ujasiri wa kusukuma mambo magumu ikiwamo suala la sera na mitaala.
“Katika miaka mitano au 10 ijayo elimu yetu itakuwa imeimarika, niwatoe shaka elimu ina malengo makubwa mawili la kwanza ni kuwezesha kujua na pili ni elimu timizi,”alisema
No comments:
Post a Comment