Serikali Yaimarisha Huduma za Uchunguzi wa Magonjwa - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, May 13, 2023

Serikali Yaimarisha Huduma za Uchunguzi wa Magonjwa


Na Immaculate Makilika – MAELEZO


Serikali imeendelea kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa lengo la kuboresha huduma za uchunguzi na utambuzi wa magonjwa kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa ili kuimarisha huduma za matibabu sahihi kwa wagonjwa na kuzisogeza karibu zaidi na wananchi.


Ambapo jumla ya mashine za MRI sita zimenunuliwa kwa gharama ya shilingi 14,534,624,000, kati ya hizo mashine nne zimeshasimikwa na kuanza kutoa huduma katika Hospitali ya Taifa-MNH, Hospitali ya Taifa ya Saratani-Ocean Road, Hospitali ya kanda-CHATO na Hospitali ya kanda-MTWARA. Usimikaji wa mashine mbili za MRI unatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 30, 2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili - MOI.


Hayo yamesemwa  Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2023/24.

 

 

“Wizara imekamilisha ununuzi wa mashine za CT scan 32 zenye gharama ya shilingi 56,465,145,570, ambapo CT Scan 24 tayari zimeanza kufanya kazi katika Hospitali za Taifa, Kanda na Hospitali Rufaa za mikoa 24 ikiwemo Kagera, Maweni-Kigoma, Iringa, Dodoma, Shinyanga, Morogoro, Tumbi-Pwani, Singida, Mount Meru-Arusha, Mwananyamala, Amana, Temeke, Hospitali Mzena (DSM), Bombo-Tanga, Sokou Toure-Mwanza, Mawenzi-Kilimanjaro, Manyara, Kitete-Tabora, Geita, Ruvuma, Rukwa, Mbeya, Njombe na Simiyu na taratibu za usimikaji CT Scan nane zinaendelea”, alieleza Waziri Ummy.


Aliongeza kuwa ununuzi wa mashine hizo umewezesha kuimarika kwa huduma za radiolojia kwa kuwa na mashine za CT Scan 45 nchi nzima kutoka 13 mwaka 2021.

 


“Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI iliratibu ununuzi wa digital x-ray 199 zenye gharama ya shilingi 44,680,031,171 ambapo digital x-ray 168 zimeshasimikwa katika vituo mbalimbali na zinaendelea kutoa huduma, usimikaji wa digital x-ray 31 bado unaendelea na utakapokamilika utawezesha sekta ya afya kuwa na jumla ya digital x-ray 346. Aidha, mashine za ultrasound 76 zenye gharama ya shilingi 4,695,000,000 zimenunuliwa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini”, alisisitiza Waziri Ummy.


Hata hivyo, idadi ya ongezeko la mashine za ultrasound 76 linafanya sekta ya afya kuwa na jumla ya mashine za ultrasound 552 kutoka 476 mwaka 2021/22.

No comments:

Post a Comment