SERIKALI YATAJA MIKAKATI YA KUONGEZA WATALII KATIKA HIFADHI YA TAIFA RUAHA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 26, 2023

SERIKALI YATAJA MIKAKATI YA KUONGEZA WATALII KATIKA HIFADHI YA TAIFA RUAHA


Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeweka wazi mikakati mbalimbali ya kuongeza watalii katika Hifadhi ya Taifa Ruaha ikiwa ni pamoja kuanzisha na kuboresha miundombinu ya barabara za ndani ya Hifadhi kwa kiwango cha changarawe na kuboresha barabara kuu kutoka Iringa Mjini mpaka hifadhini.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma leo Mei 26,2023 kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Grace Tendega aliyetaka kujua idadi ya Watalii waliotembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa mwaka 2019/2020 na mikakati ya kuongeza idadi ya watalii.


Amefafanua kuwa mikakati mingine ya kuongeza idadi ya watalii ni pamoja na kuongeza na kuboresha viwanja vya ndege saba (7) ndani ya hifadhi, kuongeza miundombinu ya malazi kwa kuongeza vitanda 263 pamoja na kutangaza maeneo ya uwekezaji.


Pia, amesema Serikali itaongeza na kuboresha mazao ya utalii kama utalii wa puto, boti, farasi, kuvua samaki, utalii wa kiutamaduni na historia, utalii wa mikutano na utalii wa michezo.


Aidha, Mhe. Masanja amesema Serikali itaongeza utangazaji wa vivutio vya utalii katika masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuvutia watalii wengi zaidi.


Akizungumzia kuhusu idadi ya watalii katika Hifadhi ya Taifa Ruaha, Mhe.Masanja amesema kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Hifadhi hiyo ilipokea jumla ya watalii 18,678 kutoka ndani na nje ya nchi.


Akijibu swali la Mbunge wa Mbinga Vijijini, Mhe.Benaya Kapinga kuhusu kupitia upya mipaka na kuweka alama katika hifadhi ya Msitu wa Litumbandosi na vijiji, Mhe. Masanja ameweka bayana kuwa Serikali inaendelea na uhakiki wa msitu huo na kwamba zitawekwa alama za mipaka zitakazoonekana ili kuwawezesha wananchi kutambua eneo la hifadhi na hivyo kuepuka migogoro.

No comments:

Post a Comment