MWANDISHI GODFRIEND MBUYA
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeanza kampeni kabambe ya kutoa elimu ya matumizi ya mionzi nchini katika taasisi za elimu kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo.
Akifundisha matumizi salama ya mionzi katika Shule ya Sekondari Makole Jijini Dodoma, msanifu wa maabara kutoka Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania Bw. Alphonce Mgina amesema mionzi inatumika nchini katika sekta ya afya, kilimo, mifugo,maji, ujenzi na maeneo mengine na TAEC ndiyo taasisi iliyopewa dhamana na serikali kuhakikisha matumizi ya mionzi yanakuwa salama kwa wafanyakazi, wananchi pamoja na mazingira.
"Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania imepewa mamlaka ya kisheria kuwalinda, wananchi dhidi ya madhara ya mionzi hivyo tunakagua vituo vinavyotumia mionzi, tunatoa leseni ya matumizi ya mionzi kwa wanaostahili na tunatoa ushauri wa teknolojia ya nyuklia na faida zake kwa nchi." amesema Mgina.
Kwa upande wake mwalimu wa somo la Fizikia kwa niaba ya Mkuu wa Shule ya Sekondari Makole Mwl. Ngegana Richard amesema ni mara ya kwanza shule yao kupata elimu ya mionzi faida zake na athari zake hivyo watakuwa mabalozi juu ya eneo la mionzi.
Aidha baadhi ya wanafunzi waliopata elimu hiyo Naomi Mbasha na Irine Abrahamu wamesema elimu ya mionzi ni vyema ikaendelea kutolewa kwani watu wengi bado haijawafikia.
No comments:
Post a Comment