Na Mwandishi wetu -Dodoma
Wakulima mkoani Dodoma wametakiwa kuhuisha taarifa zao za usajili pamoja na kusijalinkwa wakulima ambao hawajafanya hivyo ili waweze kunufaika na mbolea za ruzuku zinazoendelea kutolewa na serikali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Louis Kasera kasera amesema mfumo umeboreshwa kwani kwa sasa utaonesha aina mbalimbali za mazao yanayolimwa na mkulima ili aweze kuhudumiwa kwa mbolea kulingana na mahitaji yake kwa kuzingatia mazao anayolima.
Hayo yalibainishwa kwa nyakati tofauti tarehe 27 Mei, 2023 wakati wa mahojiano ya moja kwa moja katika studio za redio Dodoma na kikao baina ya wataalaamu kutoka TFRA ikiwa ni Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati, Joshua Ng'ondya na Mchumi Daniel Maarifa na Maafisa Ugani wa Mkoa na Wilaya za Mkoa wa Dodoma .
Louis alifafanua kuwa, mfumo uliopita ulisababisha changamoto ya wakulima kutokupata kiasi cha mbolea kinachokidhi mahitaji yao kulingana na aina ya zao linalolimwa kwani mfumo huo uliruhusu mifuko 3 kwa kila ekari moja ya shamba bila kujali ni aina gani ya zao linalolimwa.
Akifafanua juu ya imani ya wakulima wa Mkoa wa Dodoma kuwa mbolea inaharibu udongo, Kaimu Meneja wa Kanda, Joshua Ng'ondya amesema si kweli kuwa mbolea inaharibu udongo isipokuwa mkulima anapaswa kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija kwenye kilimo chao.
"Mbolea haiharibu udongo isipokuwa matumizi yasiyo sahihi ya mbolea ndiyo yanayosababisha tija isipatikane, mkulima anapaswa azingatie matumizi sahihi ya mbolea na akiona hana uelewa akutane na Afisa ugani wake ili aweze kumshauri namna bora ya kutumia mbolea". Ng'ondya alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo Mkoa wa Dodoma, Bernard Abraham aliupongeza uamuzi wa TFRA wa kukutana na wasimamizi wa kilimo katika ngazi ya mkoa na wilaya na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha azma ya kuwahudumia wakulima imefikiwa.
"Mwaka huu TFRA wamefanya vizuri sana wameamua kukutana nasi na wamekuja kwa wakati na wameheshimu sana uwepo wetu kwa kutambua kuwa sisi ndio tupo karibu na wakulima" Bernard alisisitiza.
Alisema mkoa wake umejipanga kuhakikisha wanahuisha taarifa za wakulima na kusajili wakulima wapya mapema ili kuwawezesha kupata bidhaa hiyo ifikapo Julai, 2023 na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mbolea baada ya msimu kupita.
No comments:
Post a Comment