TANESCO KUTUMIA TEKNOLOJIA YA "SOLAR PHOTO VOLTAIC" KUZALISHA MEGAWATI 150 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, May 29, 2023

TANESCO KUTUMIA TEKNOLOJIA YA "SOLAR PHOTO VOLTAIC" KUZALISHA MEGAWATI 150


Na Okuly Julius-Dodoma

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ,Leo Mei 29,2023 Jijini Dodoma imesaini Mkataba wa kuzalisha umeme Kwa jua kutumia teknolojia ya "SOLAR PHOTO VOLTAIC" wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 150 za umeme.


Huo utakuwa Mradi Mkubwa wa kuzalisha umeme Kwa kutumia jua kuwahi kutokea hapa nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Akizungumza  baada ya kushuhudia utiaji Saini wa Mkataba huo, Waziri wa Nishati Mhe.January Makamba amesema kuwa kusainiwa Kwa Mradi huo ni sehemu ya mipango ya mapinduzi katika uzalishaji wa umeme Kwa kutumia vyanzo mseto katika sekta ya Nishati nchini ili kufikia lengo la kuwa na Megawati 5000 kwenye gridi ya taifa ifikapo 2025.



“kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi tunaingiza umeme wa Jua katika gridi ya Taifa, nimpomgeze Rais wetu kwa kwa muongozo na uongozi ambao umepelekea nchi kuaminiwa na washirika wa maendeleo ikiwemo Shirika la Maendeleo la Ufaransa ambalo limetoa mkopo ambao utatekeleza mradi huu.”


Ameeleza kuwa, utekelezaji wa mradi huo wa Jua ni jitihada za Serikali za kuhakikisha inatengeneza mchanganyiko wa umeme wenye afya katika gridi ya Taifa ambao utatokana na vyanzo mbalimbali kama vile maji, gesi, upepo na Jua ili hata pale chanzo moja kinapotetereka, vyanzo vingine vitaendelea kuzalisha umeme



Akitoa taarifa ya mradi huo wa umeme Jua, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande amesema awamu ya kwanza itajumuisha ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme kwa teknolojia ya solar photovoltaic kwa ukubwa wa megawati 50 na ujenzi wa kituo kipya cha kuongeza umeme msongo wa kilovolti 33/220 ikiwa ni pamoja na kuunganisha kituo hicho kwenye gridi ya Taifa kwa msongo wa kV 220 kwenye laini ya kutoka Singida hadi Shinyanga.


"Mradi huu utatekelezwa Kwa awamu ambapo katika awamu ya kwanza zitazalishwa Megawati 50, na awamu ya pili itazalishwa Megawati 100 na Mradi huo unatarajiwa kuanza Mwezi Juni 2023 na kuchukua Miezi 14 kukamilika,"amesema Chande



Amesema kuwa mkandarasi mjenzi wa mradi huo wa Awamu ya Kwanza ni kampuni ya Sinohydro corporation ya nchini China na Mkandarasi mshauri ni kampuni ya JV Artelia ya Ufaransa na Energiovida ya Tanzania na gharama za mradi ni shilingi Bilioni 109.


Amesema kuwa mradi huo wa awamu ya kwanza utekelezaji wake hautazidi miezi 12.


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme amemshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Nishati na TANESCO kwa mradi huo na ameahidi kuwa watawapa ushirikiano wakandarasi wa mradi ili watekeleza mradi huo kwa wakati na pia kuutunza ili uweze kunufaisha wananchi wa Shinyanga na Tanzania kwa ujumla.



Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.Judith Kapinga amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya Nishati nchini


Amepongeza Wizara na TANESCO, kwa kubuni miradi mbalimbali ambayo itapelekea nchi kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika.


Kwa upande wake, Mbunge wa Kishapu, Boniphace Butondo amepongeza kwa mradi huo ambao amesema kuwa utakuwa na manufaa makubwa kwani pamoja na kupata umeme katika maeneo mbalimbali kama migodi, mradi huo utafaidisha wananchi wanaozunguka mradi kwa kupata huduma za kijamii kama shule na maji.


Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga.


Mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya "SINOHYDRO CORPORATION" kutoka China ambapo gharama za mradi Hadi kukamilika kwake ikiwemo ulipaji wa fidia Kwa wanaopitiwa na eneo la mradi ni jumla ya kiasi cha TZS 274.76 Bilioni


No comments:

Post a Comment