Asila Twaha - Katavi, Tanganyika
Wananchi Kijiji cha Majalila Kata ya Tonge Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi wameishukuru Serikali kwa kujenga Shule ya Sekondari Majalila ambayo imewapunguzia adha watoto wa eneo hilo kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Akiongea kwa niaba ya wananchi Mwenyekiti wa Kijiji cha Majalila Bw. Ally Chuma amesema kukamilika kwa shule hiyo kumewasaidia wanafunzi hao kupunguza kutembea umbali mrefu kufuata huduma na gharama za usafiri kwa wazazi.
Ameendelea kufafanua kuwa kukamilika kwa shule hiyo kumepunguza mrundikano wa wanafunzi.
“Kwakweli tulipoambiwa tunajengewa shule katika kata yetu tulishirikiana na wananchi wangu na tulifurahishwa sana na tulishirikiana kusafisha eneo lililojengwa shule hii na kusaidia shughuli nyengine ili shule ikamilike haraka” amesisitiza
Kwa upande wa Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mwl. Roza Nabahani amesema Halmashuri hiyo ilipokea sh. milioni 470 kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kujenga shule hiyo ya Sekondari kwenye maeneo yaliyo na changamoto ya ukosefu wa shule ya sekondari.
Amesema Halmashauri kwa kushirikiana na wanakijiji walihakikisha eneo linapatikana na kufuata maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali yalifuatwa.
“shule asilimia kubwa imekamilika na tumeshaisajili na sasa wanafunzi wameshaanza kusoma na wanaendelea na masomo yao na walimu wanaendelea na majukumu yao hivyo shule hii ni mkombozi mkubwa katika eneo hili sababu itasaidia mpaka kata za jirani” amesema Nabahani
Naye Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Majalila Jidala Deus amesema hivi sasa wanauwezo wa kufikia malengo yao kwasababu hakuna vikwazo vinavyoweza kuwasababishia kutokumaliza shule kwa kuwa shule hiyo imejengwa karibu na maeneo wanayoishi na inawasaidia kupata muda mwingi wa kujisomea.
Bi. Scolastika Mayene(mzazi) ameishukuru Serikali kwa kuwajengea shule katika kata yao kwa kuwa wazazi wengi itawasadia kwa kuwapunguzia gharama ya nauli
na itasaidia kuongeza ushirikiano kati yao wazazi na walimu kwa ukaribu.
No comments:
Post a Comment