WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Zedliner Global Green Economy Partnership (ZGGEP) la nchini Marekani, Donovan Griay linalojishughulisha na uwekezaji wa Biashara ya Kaboni duniani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Mei 11, 2023 katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mtumba jijini Dodoma, Dkt. Jafo amewahakikishia wawekezaji hao utayari na ushirikiano kutoka Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ajili ya kuanzisha miradi ya uwekezaji wa Biashara ya Kaboni nchini.
Dkt. Jafo amemueleza Rais wa ZGGEP biashara ya kaboni kama nyenzo muhimu katika kukuza uchumi na kuibua fursa za maendeleo kwa wananchi ambapo kutokana na umuhimu huo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Taasisi nyingine za Umma imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na mapitio ya sera, uandaaji wa kanuni, mikakati na miongozo.
Waziri Jafo amesema Malengo makuu ya Kanuni na Mwongozo hiyo ni pamoja na kuweka utaratibu na masharti ambayo wadau na wajasiriamali wa biashara ya kaboni watapaswa kuzingatia wakati wa utekelezaji wa miradi mipya na miradi inayoendelea ya biashara ya kaboni katika sehemu mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kanuni na mwongozo huu unalenga kuweka mazingira rafiki ya usimamizi wa mazingira na biashara yaKaboni. Tunawakaribisha wawekezaji na milango yetu ya ushirikiano ipo wazi, tuna maeneo makubwa ya misitu, na maeneo mengine ya uoto wa asili yanayofaa kwa ajili ya biashara ya kaboni” amesema Dkt. Jafo katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na wataalamu wa Ofisi ya Makamu wa Rais na wawekezaji wazawa kutoka Kampuni za Global International na GIS.
Akifafanua zaidi Dkt. Jafo amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu na Taasisi za Umma itaendelea kuimarisha mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji wa biashara ya kaboni ikiwemo kuimarisha mifumo ya usajili wa makampuni ya uwekezaji wa biashara ya kaboni hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Dkt. Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Idara ya Mazingira kwa kushirikiana na Wizara za kisekta, Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa jamii, na wadau mbalimbali wanaohusika na biashara hiyo ikiwa pamoja na inanufaika kikamilifu kutokana na faida zilizopo katika biashara ya kaboni nchini.
Kwa upande wake, Rais wa Shirika la ZGGEP Donovan Griay ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa hatua kubwa iliyofikia katika uendelezaji wa biashara ya kaboni nchini na kueleza utayari wa Shirika hilo kuja kuwekeza nchini kwa kuanzisha miradi ya biashara ya kiuchumi na kuibua fursa kwa jamii.
“Tupo tayari kuwekeza na tumejipanga kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa biashara ya kaboni inaibua fursa ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi” amesema Griay.
Itakumbukwa kuwa Tanzania ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris inayotekeleza Biashara ya Kaboni.
No comments:
Post a Comment