DKT.MPANGO AZIONYA HALMASHAURI UTOAJI WA MIKATABA KWA MAKAMPUNI YA USAFI YASIYO NA SIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 5, 2023

DKT.MPANGO AZIONYA HALMASHAURI UTOAJI WA MIKATABA KWA MAKAMPUNI YA USAFI YASIYO NA SIFA


Na Okuly Julius-Dodoma

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Philip Mpango amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuacha tabia ya kutoa mikataba ya usafi wa Mazingira kwa Makampuni yasiyo na uwezo wala sifa.


Dkt.Mpango amesema kuwa unakuta kampuni imepewa mkataba wa kufanya usafi ila  magari yanayotumika kuzoa taka nayo ni takataka.



Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo mara baada ya kuongoza zoezi la kufanya usafi katika soko kuu la wamachinga mjini Dodoma ikiwa ni katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani leo tarehe 5 Juni 2023.


Amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kuongeza nguvuzaidi katika kusimamia utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini.



Amesema ni
lazima kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa kwa wanaokiuka maagizo
hayo pamoja na kuwataka watendaji wote wanaohusika kusimamia kwa
karibu uzalishaji na matumizi ya mifuko mbadala.



Makamu wa Rais ameongeza kwamba ni vema kuhakikisha mifuko yote
inayozalishwa inaonesha taarifa za mzalishaji na kama inakidhi viwango
vilivyowekwa na mamlaka husika. 


Pia amesisitiza makampuni na watu binafsi
wanaozalisha bidhaa za plastiki kuhakikisha taka zinazotokana na bidhaa
zinazozalishwa zinakusanywa na kuondolewa.



Amekemea utoaji wa tenda za uzoaji taka kwa kampuni
zisizokuwa na uwezo na zile zisizo na vitendea kazi vya kisasa na kuzitaka
Halmashauri kuweka miundombinu ya uhakika ya ukusanyaji na usombaji wa
taka katika mitaa na maeneo ya mikusanyiko kama sokoni, stendi na
hospitalini.


Aidha Dkt. Mpango ametoa wito kwa wananchi kutambua wajibu walionao
katika kutunza vyanzo vya maji, kuacha mazoea ya kutupa taka hovyo na
kuagiza kila kaya kuwa na sehemu mahsusi ya kuhifadhia ama kuchomea
taka. Amesema masuala ya kufanya usafi na utunzaji mazingira hayana
mbadala kwa kuwa mazingira ndio uhai na yana mahusiano ya moja kwa
moja na ustawi wa Taifa kiuchumi na kijamii.



Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema suala la utunzaji na uhifadhi wa
mazingira limeendelea kupewa kipaumbele hapa nchini ambapo kwa kutumia
Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kauli mbiu iliopo ni yenye lengo la kuhamasisha ajenda ya utunzaji wa mazingira na kutunza vyanzo vya maji.


Dkt Jafo amewapongeza wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu
kwa kujitoa kihifadhi mazingira ikiwemo kampeni ya soma na mti yenye lengo
la kuhamasisha upandaji wa miti mashuleni. Halikadhalika amewashukuru wadau mbalimbali katika jitihada zao za kuhakikisha suala la mazingira
linapewa kipaumbele kwa maendeleo endelevu.



Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema mkoa huo
unaendelea na kampeni ya kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki ambapo
tayari kwa kushirikiana na NEMC waliweza kukifungia kiwanda kimoja
kinachozalisha mifuko hiyo.


Amesema elimu inaendelea kutolewa katika
masoko na maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanaachana na
matumizi ya mifuko hiyo.



Pia ameongeza kwamba Mkoa huo utaendelea na jitihada za kulinda vyanzo
vya maji ikiwemo chanzo cha maji Mzakwe kwa kusimamia na kupanda miti
katika eneo hilo muhimu.


Amesema mkoa utaendeleza hamasa ya usafi wa
mazingira iliofanyika katika wiki ya kuadhimisha siku ya mazingira duniani
hususani usafi katika mifereji ya jiji la Dodoma.


Zoezi la kufanya usafi katika soko kuu la wamachinga mjini Dodoma
limewashirikisha viongozi mbalimbali, wananchi na watumiaji wa soko hilo.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka 2023
inasema “Shinda uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki”



Naye Chifu wa Kabila la Wagogo Chifu Lazaro Masuma Chihoma ameipongeza Serikali Kwa kuendeza agenda ya Uhifadhi wa Mazingira kwani Kwa upande wao Machifu agenda ya utunzaji wa Mazingira ni ya Kudumu.


"Sisi kama Machifu tutaendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya Uchafuzi wa Mazingira ili Serikali hii ya awamu ya Sita Inayoongozwa na Dkt.Samia ifanikiwe katika katika utunzaji wa Mazingira.


No comments:

Post a Comment