WAOMBAJI WA AJIRA 86,448 WAKIDHI VIGEZO,WAINGIZWA KWENYE MCHAKATO WA KUPANGIWA VITUO VYA KAZI-MHE.KAIRUKI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 5, 2023

WAOMBAJI WA AJIRA 86,448 WAKIDHI VIGEZO,WAINGIZWA KWENYE MCHAKATO WA KUPANGIWA VITUO VYA KAZI-MHE.KAIRUKI


Na Okuly Julius-Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Mhe.Angellah Kairuki amesema Jumla ya maombi ya ajira 171,916 yakiwemo ya Wanawake 76,190 na Wanaume 95,726 yalipokelewa kwenye mfumo, ambapo maombi ya Kada za Afya yalikuwa ni 48,705 na Kada ya Ualimu ni 123,211.


Ambapo baada ya zoezi la uhakiki wa waombaji kimfumo na mapitio ya nyaraka, jumla ya waombaji 86,448 walikidhi vigezo vyote na hivyo kuingizwa katika mchakato wa kupangiwa vituo vya kazi.


Akitoa Taarifa mbele ya waandishi wa habari Leo Juni 5,2023 Jijini Dodoma Mhe.Kairuki amesema kuwa kati ya waombaji 86,448 waliokidhi vigezo, waombaji wa kada za Afya ni 21,273 ambao kati yao wanawake ni 10,618 na wanaume ni 10,655. Aidha, waombaji wa kada ya Ualimu 65,175 walikidhi vigezo, ambao kati yao wanaume ni 38,584 na wanawake ni 26,591.


"Waombaji 86,448 waliokidhi vigezo na sifa walitakiwa kujaza nafasi za kazi 21,200 (Ualimu 13,130 na Afya 8,070) kwa mujibu wa Kibali kilichotolewa. Hata hivyo, mchakato wa kukamilisha uchambuzi wa maombi katika jumla ya nafasi 2,751 za kada ya afya unaendelea, na utatangazwa punde utakapokamilishwa,


Na kuongeza kuwa "Upangaji wa waombaji waliokidhi vigezo kwenye vituo vya ajira umezingatia vigezo na utaratibu uliobainishwa katika kipengele cha 2.1 hadi 2.3. Kwa kuzingatia vigezo hivyo, jumla ya waombaji 18,449 wamechaguliwa na kupangiwa vituo vya kazi. Kati ya waombaji 18,449 waliochaguliwa na kupangiwa vituo, kada za afya ni 5,319 na kada za Ualimu ni 13,130,"amesema Kairuki




Akitoa Mchanganuo wa nafasi hizo amesema kwa upande wa kada za Ualimu, waombaji waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 13,130, ambapo jumla ya walimu 7,801 wamepangwa shule za Msingi na walimu 5,329 Shule za sekondari. Kati ya waombaji 13,130 waliopata ajira, waombaji wenye uhitaji Maalum ni 111 sawa na asilimia 0.84, ambapo wanawake ni 36 na wanaume 75.


Kwa upande wa Waliochaguliwa na Kupangiwa Vituo Kada za Afya Jumla ya waombaji waliopangiwa vituo kada za afya ni 5,319 ambapo wanawake ni 2,138 sawa na asilimia 40 na wanaume ni 3181 sawa na asilimia 60. Idadi hii ya waajiriwa wa kada ya afya wamo pia wenye uhitaji Maalum 92 sawa na asilimia 1.7 ambapo kati yao wanawake ni 46 na wanaume ni 46.




Mhe.Kairuki ameongeza kuwa upangaji wa watumishi wa Kada za Afya na Ualimu katika Vituo vya kutolea huduma za Afya na shule umezingatia mahitaji ya watumishi katika Halmashauri husika, uwepo wa Shule au vituo vipya vya kutolea huduma za afya, uwepo wa vifaa tiba kama vile xray mashine zenye kuhitaji watumishi maalum na kutokuwepo baadhi ya walimu wa masomo katika shule mbalimbali.



MAELEKEZO YA MHESHIMIWA WAZIRI WA NCHI-OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA)

Waajiriwa wapya, kabla ya kuripoti kwenye vituo vya kazi walivyopangiwa, wanatakiwa kuripoti kwa Wakurugenzi wa Halmashauri wakiwa na:-


Kitambulisho cha Taifa au namba ya utambulisho ya NIDA;
Cheti halisi cha kuzaliwa;


Vyeti Halisi (Original Certificates) vya Kidato cha Nne, Sita, Chuo Kikuu, NACTE, Leseni hai na vyeti halisi vya usajili wa mabaraza ya kitaalam kwa ajili ya kuhakikiwa na mwajiri kabla ya kupewa barua ya ajira.
Waajiriwa Wapya waripoti na kufanya kazi kwenye vituo walivyopangiwa;


Mwajiriwa mpya atakayechukua posho ya kujikimu na baadaye asiripoti katika kituo chake cha kazi alichopangiwa atachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kushitakiwa kwa kosa la kujipatia fedha/ mali kwa njia ya udanganyifu;


Waajiriwa wapya ambao hawataripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya tangazo hili, watakuwa wamepoteza nafasi zao na nafasi hizo zitajazwa na waombaji wengine wenye sifa waliopo kwenye Kanzidata (Database) ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI.


Waajiriwa wapya hawaruhusiwi kubadilisha kituo na kuomba Uhamisho kabla ya kutimiza miaka mitatu, watatakiwa kusaini mkataba wa kufanya kazi katika vituo hivyo si chini ya miaka mitatu.

MAELEKEZO KWA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI.


Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo Waajiriwa wapya wamepangiwa kuhakikisha kuwa:


Wanawapokea watumishi wapya waliopangwa kwao na kuwawezesha kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma na baadaye kutoa taarifa ya kuripoti kwa watumishi hao.


Wanaandaa taarifa ya kuripoti waajiriwa hao kwenye mfumo wa kielektroniki (ajira.tamisemi.go.tz) baada ya kila mtumishi kupokelewa na kukamilisha taratibu.

Wanakamilisha taratibu za ajira za waajiriwa wapya kwenye mfumo wa malipo ya mshahara (Payroll) mapema iwezekanavyo.


KUJUA MATOKEO YA MAOMBI

Majina ya waombaji wote waliopangiwa vituo vya kazi yanapatikana katika Tovuti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kiunganishi cha:

www.tamisemi.go.tz.


Waombaji wote ambao majina yao hayakuonekana katika tangazo hili, watambue kuwa hawakupata nafasi hivyo wasisite kuomba kwa mara nyingine nafasi za kazi zitakapotangazwa.


Ikumbukwe kuwa mwezi Aprili, 2023; Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa kibali cha ajira ya watumishi 21,200 kati yao 13,130 walikuwa wa kada ya Ualimu na 8,070 wa kada za Afya.

No comments:

Post a Comment