MAKAMPUNI YA ULINZI BINAFSI YAOMBA SHERIA MAALUMU YA KUSIMAMIA SEKTA HIYO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, January 20, 2026

MAKAMPUNI YA ULINZI BINAFSI YAOMBA SHERIA MAALUMU YA KUSIMAMIA SEKTA HIYO



Mwenyekiti wa Umoja wa Kampuni Binafsi za Ulinzi Tanzania Kanda ya Kati (UKUTA), Isaya Saimon Momba, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya GOSHEN Tanzania,akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 20, 2026 jijini Dodoma.


Na Okuly Julius, OKULY BLOG – Dodoma


Makampuni ya ulinzi binafsi nchini yameiomba Serikali kuunda sheria maalumu itakayosimamia sekta ya ulinzi binafsi badala ya kuendelea kutegemea kanuni zilizopo kwa sasa ambazo zinasimamiwa chini ya Jeshi la Polisi Tanzania.

Ombi hilo limetolewa kutokana na changamoto mbalimbali zinazozikabili kampuni hizo, ikiwemo ucheleweshaji wa vibali vya kumiliki silaha, kukosekana kwa mwongozo wa bei elekezi, pamoja na ukosefu wa mwelekeo mmoja wa kisheria unaoratibu masuala ya maslahi ya wafanyakazi na michango ya lazima.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 20, 2026 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Umoja wa Kampuni Binafsi za Ulinzi Tanzania Kanda ya Kati (UKUTA), Isaya Saimon Momba, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya GOSHEN Tanzania, amesema kupatikana kwa sheria maalumu kutaleta mapinduzi makubwa katika tasnia hiyo.

Amesema kwa sasa vibali vya kumiliki silaha huchukua muda mrefu kupatikana, hali inayokwamisha utekelezaji wa majukumu ya kampuni za ulinzi binafsi, huku kukiwa pia hakuna mwongozo wa wazi kuhusu viwango vya mishahara ya walinzi na michango mbalimbali ya kisheria.

Momba ameeleza kuwa, kupitia kampeni maalumu inayoandaliwa na Kampuni ya ulinzi ya GOSHEN & RIPPLE A SECURITY AGENCY , kutakuwa na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Geita, ambao watatoa elimu na kufanya usajili wa wanachama wapya. Aidha, Polisi Jamii watatoa mafunzo kuhusu masuala muhimu ya ulinzi na usalama.

Ametoa wito kwa wadau wote wanaopata huduma za ulinzi kutoka kampuni ya GOSHEN na nyinginezo kuzipokea mabadiliko hayo kwa mikono miwili ili kuepuka migongano isiyo ya lazima na Serikali pindi kampuni zitakapokiuka maelekezo ya kisheria kwa kukosa uelewa wa kutosha.

Katika maombi yao kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, makampuni ya ulinzi binafsi yameainisha mambo manne muhimu ikiwemo kupatikana kwa sheria ya kusimamia tasnia ya ulinzi binafsi, hatua itakayosaidia kuwepo kwa bei elekezi, kuundwa kwa chama kimoja cha kitaifa kitakachounganisha sekta hiyo badala ya vyama vingi visivyo na sauti moja, pamoja na kurahisisha upatikanaji wa vibali vya kumiliki silaha kwa wakati.

Kwa mujibu wa Momba, kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Februari 2, 2026 katika Mkoa wa Geita, Wilaya ya Bukombe, katika viunga vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bukombe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Paskasi Mragili.


Makampuni hayo yanaamini kuwa kupatikana kwa sheria maalumu kutaimarisha usalama, kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuongeza ufanisi wa sekta ya ulinzi binafsi nchini.

No comments:

Post a Comment