ELIMU YA KUZUIA RUSHWA YAWAFIKIA WAFUNGWA DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 22, 2023

ELIMU YA KUZUIA RUSHWA YAWAFIKIA WAFUNGWA DODOMA


Na Mwandishi wetu -Dodoma


Katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Dodoma imewataka wafungwa wa gereza la Msalato kuwa mstari wa mbele kufichua vitendo vya rushwa vinavyojitokeza kwenye maeneo yao.


Haya yameelezwa Juni 21, 2023 na Afisa TAKUKURU Faustine Malecha wakati akitoa elimu ya rushwa kwa wafungwa wa gereza hilo.


“Ni wajibu wako wa kutoa taarifa rushwa inapotokea. Unawajibu wa kutoa ushahidi mahakamani pale inapokulazimu kufanya hivyo. Kutoa taarifa ya rushwa ni lazima useme. Kila mwananchi anawajibika kutoa taarifa za vitendo vya rushwa popote pale alipo,” alisema Malecha.


Aidha, alisema kuna wengine wako gerezani kwa sababu tu walishindwa kutimiza masharti hali iliyopelekea kuendelea kuwepo gerezani.


“ Kwanza niwaambie dhamana ni bure ili mradi utimize masharti. Watu wanadhani dhamana ni kutoa fedha hapana, dhamana ni haki yako,” aliongeza.


Kutokana na changamoto zinazowakabili wafungwa gerezani, Malecha aliishauri Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuwa na utaratibu wa kutembelea magereza kusikiliza changamoto zinazowakabili.


“ Tume ya Haki za Binadamu inawajibu wa kusikiliza changamoto za wafungwa.” alisisitiza.


Baadhi ya wafungwa wa gereza hilo, walieleza kuwa rushwa imesababisha baadhi yao kufikishwa gerezani. Walisema Serikali isipochukua hatua za haraka kukabiliana na vitendo vya rushwa sehemu za kutoa haki, itatengeza taifa la watu wenye chuki na nchi yao.


Kwa upande wa Sabeth Mshana Afisa TAKUKURU alisema, licha ya changamoto wanazopitia wafungwa gerezani bado wanayo nafasi ya kutoa taarifa za rushwa ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wale watakao kutwa na hatia.


“Ni muhumi kutoa taarifa tujue, hii nchi ni yetu wote. Usipokuwa mzalendo unaiua nchi yako. Palipo na rushwa hakuna haki. Wapo watu wanateseka kwa kutokujua na kupata elimu ya ruswa. Tunatoa elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa lengo ni kufikisha ujumbe kwa wananchi.” alisema Sabeth.


Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya 2007, iliyotungwa kwa shabaha ya kuanzisha na kuipa nguvu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inalenga kushughulikia kikamilifu makosa ya rushwa na yale yanayofanana nayo hapa nchini.

No comments:

Post a Comment