PROF.MKENDA "ONENI UMUHIMU WA KUIMARISHA UBORA WA ELIMU" - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 2, 2023

PROF.MKENDA "ONENI UMUHIMU WA KUIMARISHA UBORA WA ELIMU"


Na Mwandishi wetu Dar es salaam

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ametoa wito kwa Vyuo Vikuu nchini kuona umuhimu wa kuimarisha ubora wa elimu ya juu ili iweze kuakisi mahitaji ya nchi na watu.


Waziri Mkenda ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga warsha ya kubadilishana uzoefu kwa Wenyeviti na Wajumbe wa Mabaraza, Seneti na Bodi za Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki ambapo amesema lengo ni kuwa na wahitimu bora.



Pia amevishauri Vyuo kuona ni namna gani wanaweka viwango vinavyofanana vya ubora kwa vyuo Vikuu vyote na kwamba kama hilo lisipofanikiwa kuwepo na gredi ambazo zitakuwa zikitumiwa na Vyuo Vikuu.


“Kuweka viwango itasaidia mhitimu wa Chuo A asionekane ni tofauti na wa Chuo B ili wawe na nafasi sawa za ajira. Msukumo mkubwa wa Vyuo ni kuwa na wanafunzi wengi, ninawaomba _tusicompromise_ ubora wa elimu,”amesema Prof. Mkenda



Ameongeza kuwa kazi ya Vyuo Vikuu ni kuzalisha na kusambaza uelewa hivyo wahadhiri wa Vyuo vikuu lazima wawe wanafanya kazi za tafiti ili kutafuta ugunduzi mbalimbali wakati wanafundisha.

“Vyuo ni lazima viendele kujenga mazingira mazuri ya wahadhiri wake kufanya utafiti vipo baadhi ya Vyuo ambavyo inaonekana mtizamo wake ni kama utafiti ni chanzo cha mapato haiwezi kuwa hivyo na haitakiwi kuwa hivyo utafiti ni chanzo cha maarifa kwa hiyo lengo la utafiti kwa vyuo vikuu ni kuwa na maarifa mapya,”amesisitiza Prof. Mkenda


Akizungumzia mageuzi ya elimu yanayofanyika nchini Prof Mkenda amevitaka Vyuo Vikuu kuona umuhimu wa kuandaa walimu kwa ajili ya kufundisha katika mkondo wa Elimu ya Amali. Lengo ni shule za Ufundi zitakapoanza kutoa elimu ya ufundi kuwe na walimu waliosoma ualimu lakini wamesomea na mafunzo ya Amali mfano Uhandisi na Kilimo.


"Kuelekea kwenye kufufua shule zetu za ufundi ni lazima tuandae walimu kwa ajili ya kwenda kufundisha mafunzo ya Amali hivyo vyuo vinavyotoa Kozi ya ualimu waongeza na mafunzo ya Amali kwa mfano Chuo Kikuu Cha Sokoine wanatoa Ualimu na Kilimo hivyo tayari mwalimu akimaliza anaweza kufunduasha Mafunzo ya Amali," ameeleza Prof.Mkenda

Akizungumzia ujenzi wa Kampasi mpya za Vyuo Vikuu zinazojengwa na Mradi wa HEET Waziri Mkenda amesema Vyuo vione umuhimu kampasi hizo kutoa shahada ya elimu ya Amali akitolea mfano DIT na ATC ambavyo vinatoa shahada hizo , lengo ni kuyaongezea mafunzo hayo wigo ili yamwandae mhitimu kuanza kazi haraka zaidi.


Akizungumza kwa niaba ya washiriki Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) Dkt. Harrison Mwakyembe amemueleza Waziri Mkenda kuwa msisitizo Mkubwa katika warsha hiyo ilikuwa ya elimu kwa vitendo na kushukuru waandaaji wa warsha hiyo.


Dkt. Mwakyembe amemuomba Waziri Mkenda kusaidia MUHAS ili hospitali ya Mloganzila iweze kurudi kuwa ya Chuo ili wanafunzi waweze kusoma kwa vitendo na kupata wahitimu bora zaidi.


Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania Prof. Charles Kihampa amesema warsha hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa washiriki wamepitishwa kwenye mada ambazo zina lenga katika kuendelea kuimarisha ubora wa elimu ya juu.

No comments:

Post a Comment